1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya Mudhoon Loay juu ya Muhammed Mursi

Abdu Said Mtullya25 Juni 2012

Kwa mara ya kwanza katika historia yake ya hivi karibuni, Misri imepata Rais aliechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Ni Muhammed Mursi wa chama cha udugu wa kiislamu.

https://p.dw.com/p/15LBm
Rais mteule wa Misri Muhammed Mursi
Rais mteule wa Misri Muhammed MursiPicha: AP

Ushindi wa Muhammed Mursi maana yake ni kwamba, kwa mara ya kwanza Misri itaongozwa na Rais ambae si mwanajeshi tokea kumalizika kwa ukoloni.

Katika kipindi cha miezi 16 ya harakati za kuleta mapinduzi, Misri,yaani moyo wa dunia ya kiarabu ni nchi iliyogawanyika kisiasa. Mkakati wa kundelea na harakati za mapinduzi kwa muda mrefu,na wasiwasi uliosababishwa na majenerali uliwachokesha Wamisri wa kawaida waliosimama katika upande mwingine wa mstari wa mbele wa harakati zilizoendelea kwenye uwanja wa Tahrir.

Hali hiyo imesababisha kiwango kikubwa cha kuungwa mkono kwa Ahmed Shafik - yaani mwakilishi fisadi wa utawala wa Mubarak. Alishindwa kwa kura chache katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Idadi kubwa ya jumuiya zilizoongoza harakati za mapinduzi zilimuunga mkono Muhammed Mursi katika wiki za mwisho siyo kwa sababu ya kukubaliana na itikadi yake, bali kwa sababu ya kutaka kuondokana kabisa na utawala wa Mubarak.

Na kusema kweli ushindi wa Muhammed Mursi ulikuwa ukomeshe utawala wa kijeshi uliodumu kwa muda wa miaka 60 nchini Misri. Lakini Rais huyo mtuele hatakuwa na maamlaka yoyote baada ya baraza la kijeshi la Misri kulivunja bunge lililochaguliwa kwa njia za kidemokrasia.Baraza la kijeshi la Misri ndilo litakalokuwa na mamlaka juu ya bajeti na litachukua mahala pa bunge.Ni wazi kwamba baraza la kijeshi lilipendelea Shafik awe Rais wa Misri. Iwapo angelikuwa Rais,marupurupu ya maafisa wa jeshi chini ya jemadari Tantawi yangeliendelezwa kwa urahisi.

Majenerali wamemkubali Mursi kuwa mshindi kutokana na kuhofia upinzani wa wananchi endapo wangejaribu kula njama za kumpa ushindi mjumbe wao Shafiq.Walihofia ghasia kubwa ambazo zingeliweza kwenda mrama na kutoweza kudhibitika. Watu wengi mashuhuri ,hasa wanasiasa wa kambi ya upinzani, ikiwa pamoja na mshindi wa nishani ya amani ya Nobel Mohammed Elbaradei ,katika siku za mwisho waliowaonyesha majenerali, ni kwa kiasi gani mambo yangelikuwa ya moto .

Hata hivyo Rais Mtuele, Muhammed Mursi atawategemea wanaharakati wa uwanja wa Tahrir ikiwa atataka kufanikiwa katika mtihani wake na majenerali. Kwani Misri haitakuwa na mustakabal wowote bila ya kuuangusha mhimili wa mamlaka ya wanajeshi na tishio la waislamu wenye itikadi kali.

Mwandishi:Mudhoon,Loay

Tafsiri:Mtullya Abdu

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman