1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI JUU YA BERLUSCONI

Abdu Said Mtullya9 Novemba 2011

Wahariri watoa maoni juu ya Berlusconi.

https://p.dw.com/p/137iS
Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi.Picha: dapd

Katika ripoti yake Shirika linalodhibiti matumizi ya nishati ya nyukilia dunia, IAEA limeonyesha wasi wasi mkubwa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Mhariri wa gazeti la Fuldaer Zeitung anatoa maoni yake juu ya ripoti hiyo kwa kusema kuwa Shirika hilo halijawahi kuwa wazi kwa kiasi hicho. Mhariri huyo anasema hata kama Shirika hilo bado halijaweza kuupata ushahidi thabiti juu ya mipango ya Iran ya kuunda silaha za nyuklia, ripoti yake ipo wazi kabisa. Sasa ni juu ya marafiki wa Iran, China na Urusi kumweka sawa rafiki yao Mahmud Ahmadinejad. Diplomasia bado inaweza kutumika.!

Mhariri wa Badische Zeitung anamzungumzia Waziri Mkuu wa Italia Silvio Bersconi kwa kutilia maanani kwamba watu wake sasa wanamtaka Waziri Mkuu huyo afunge virago haraka!

Mhariri wa gazeti hilo anasema Stahamala juu ya Berlusconi imefikia mwisho miongoni mwa wananchi wa Italia. Sasa watu hao wanamwambia kiongozi wao kwa kitaliani, "Basta"yaani inatosha!Ondoka bwana. Hata hivyo gazeti la Badische linasema jambo muhimu ni kwa serikali itakayokuja kuyatekeleza masharti yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya-yaani kuleta mageuzi katika sekta ya uchumi na kuchukua hatua za kubana matumizi.

Gazeti la Donaukurier pia linatilia maanani kwamba,sasa wakati umefika kwa Berlusconi kuondoka,lakini gazeti hilo,wakati huo huo, linawaluamu watu wa Italia kwa kucheza mchezo wa Mbuni pamoja na viongozi wao-kwa kujifukia vichwa ardhini na kutoona hali halisi.

Gazeti hilo linaeleza kuwa ni vigumu kuamini kwamba Berlusconi mwenyewe, sasa anaurudisha upanga katika ala, kuashiria mwisho wa mapambano. Hata hivyo hana nia ya kuondoka haraka. Amesema anataka kuiweka Italia katika njia ya mageuzi.Lakini nani asiyemjua Berlusconi gazeti linauliza? Bado anaweza kuendelea madarakani kwa muda mrefu. Italia ni nchi iliyolemewa na zigo kubwa la madeni-madeni yaliyokuwa yanalimbikizwa kwa muda wa miaka mingi. Wataliani walipaswa kuziona ishara siku nyingi, lakini wao pia wamewafuata viongozi wao katika kucheza mchezo wa Mbuni, kujifukia vichwa ardhini na kutouona ukweli.

Naye mhariri wa Nordwest Zeitung anasema miaka 17 ya Berlusconi madarakani ilikuwa sawa na kujaribu kuchota maji kwa kutumia pakacha. Ilikuwa kazi bure!

Mhariri wa gazeti hilo anasema katika muda wote huo jina la Berlusconi liliandamana na kashfa kem kem. Hakuwa tafauti sana na watawala dhalimu katika nchi za Kiarabu ambao hawakutaka kuona hali halisi mpaka walipotimuliwa. Sasa hakuna kinachoweza kumsaidia Berlusconi, hakika yeye ni mwanasiasa wa kusikitisha!

Mwandshi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Othman Miraj/