1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya hotuba ya Obama

Abdu Said Mtullya11 Septemba 2013

Wahariri wanatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria na kuchaguliwa kwa Thomas Bach wa Ujerumani kuwa Rais wa Kamati ya kimataifa ya Olimpiki.

https://p.dw.com/p/19fum
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: Getty Images

Gazeti la "Der neue Tag" linaanza kwa habari za kutia moyo kutoka Marekani.Rais Obama jana alitoa hotuba juu ya mgogoro wa Syria ambapo watu walimtarajia Rais huyo autumie wasaa wa hotuba hiyo kuunadi mpango wa kuishambulia Syria. Lakini mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" anasema Obama alibadilika kutoka kuwa kipanga mshambulizi, na kuwa njiwa wa amani. Mhariri huyo anasema Obama alizungumzia juu ya amani na kuamua kuuweka kando mpango wa mashambulizi angalau kwa sasa. Gazeti hilo linasema njia yoyote nyingine ni bora kuliko kuishambulia Syria bila ya kujua matokeo yake yatakuaje.

Gazeti la "Aachener" pia linautilia maanani mrengo wa amani katika hotuba ya Rais Obama. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba watu wote wametoa pumzi ya faraja.Kila mtu anaomba pawepo njia ya amani katika kufikia suluhisho la mgogoro wa Syria. Hata hivyo anasema ni mapema mno kuzungumzia juu ya suluhisho kwani Assad anaweza kufanya chochote, na mshirika wake mkuu Rais Putin wa Urusi ni mgeugeu.

Suluhisho kwa shinikizo la Putin

Mhariri wa "Rhein-Necker "anasema suluhisho litapatikana Syria ikiwa Rais Putin atakuwa tayari kuendeleza shinikizo kwa Rais Assad. Na gazeti la "Darmstädter Echo" linasema vita vya nchini Syria vimeshababisha vifo vya maalfu kwa maalfu ya watu na mauaji hayo yataendelea hata baada ya Assad kuziweka silaha zake za sumu chini ya udhibiti wa jumuiya ya kimataifa.

Rais mpya wa IOC

Thomas Bach wa Ujerumani amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki. Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linasema sasa ni juu yake kuonyesha kwamba anastahili heshima aliyopewa.

Na mhariri wa gazeti la "Badische" anauliza jee Rais huyo mpya wa IOC atapambana na uovu wa matumizi ya dawa za kuongeza nguvu katika michezo? Gazeti hilo linaeleza kwamba Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki,IOC inaweza kutoa ishara ya nguvu katika harakati za kupambana na wanariadha wanaotumia dawa za kujiongezea nguvu za misuli.

Mhariri anasema kamati hiyo inaweza kuanzisha taratibu maalumu za kupambana na uovu huo kwa kuzinyima ruhusa ya kushiriki katika mashindano, nchi ambazo hazishiriki katika harakati za kupambana na uhalifu huo.Lakini swali sasa, ni jee Rais huyo mpya Thomas Bach kutoka Ujerumani atauanzisha mjadala juu ya suala hilo? Na gazeti la "Freie Presse " linasema Kamati ya IOC imefanya uamuzi sahihi kwa kumchagua Thomas Bach.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: