1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya kujiuzulu kwa Rais Köhler.

Abdu Said Mtullya1 Juni 2010

Wahariri wa magezti leo wanatoa maoni yao juu ya kujiuzulu kwa rais Horst Köhler.

https://p.dw.com/p/Nf9o
Rais wa Ujerumani Horst Köhler amejiuzulu.Picha: AP

Rais wa Ujerumani Horst Köhler amejiuzulu, hatua ambayo imewashtua na kuwashangaza wajerumani karibu wote.

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya hatua ya rais huyo.

Gazeti la General Anzeiger linasema mtu anapaswa kuuheshimu uamuzi wa rais Köhler. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema mtu pia anayo haki ya kuuliza iwapo alichofanya Horst Köhler ni sawa: yaani kujiondoa katika wajibu kwa njia hiyo!

Gazeti la Die Welt linasema Horst Köhler ameondoka katika namna ya kusikitisha, katika namna ambayo hakustahili. Gazeti hilo linaeleza kwamba Horst Köhler amejiuzulu akiwa amevunjika moyo sana.

Alitaka kuwa rais wa wajerumani wote. Na ndiyo sababu alitembea nchini Ujerumani kote, lakini mwishowe alipaswa kutambua kwamba hakuwapo mahala sahihi!

Hata hivyo mhariri wa gazeti la Reutlinger General-Anzeiger anasema sababu za kujiuzulu kwa rais Köhler zina mizizi mirefu zaidi.

Mhariri huyo anasema ni kweli kwamba rais Köhler alipendwa na wananchi, lakini wakati huo huo alihisi kuwa aliwekwa nje ya makao makuu ya siasa za Ujerumani.Mazingira hayakuwa ya kumchangamkia rais huyo. Kuondoka kwake ni jambo la kusikitisha.

Lakini mhariri wa gazeti la Der neue Tag anasema ikiwa pana jambo lililovuruga hadhi ya ofisi ya rais, basi ni namna jinsi rais huyo alivyong'atuka na siyo lawama zilizotolewa juu ya kauli yake kuhusu Afghanistan. Na mhariri wa gazeti la Cellesche anaongezea kwa kusema, ndiyo Horst Köhler alitoa kauli juu ya majukumu ya jeshi la Ujerumani, na pia ni kweli kwamba alikosolewa vikali,lakini hiyo siyo sababu ya kumfanya rais wa Ujerumani ajiuzulu. Mhariri wa Cellesche anatuhumu kwamba bwana Köhler alikuwa anatafuta sababu ya kujing'atua

Gazeti la Mitteldeutsche linahoji kuwa bwana Köhler amechagua kuondoka wakati mbaya.Ameondoka wakati ambapo Ujerumani inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi usiokuwa na mithili tokea kuundwa kwa jamhuri hii baada ya kumalizika kwa vita kuu vya pili. Gazeti la Mitteldeutsche linatilia maanani kwamba Horst Köhler ameachia ngazi wakati ambapo,siyo tu, sarafu ya Euro imo hatarini bali jumuiya nzima ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi/Mtullya/Deutsche Zeitungen/.Mhariri/Abdul-Rahman