1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI JUU YA KUJIUZULU ROLAND KOCH

Abdu Said Mtullya26 Mei 2010

Waziri Mkuu wa jimbo la Hesse Roland Koch ametangaza kujiuzulu

https://p.dw.com/p/NY11
Waziri Mkuu wa jimbo la Hesse Roland Koch ang'atuka!Picha: AP

Waziri Mkuu wa jimbo la Hesse lililopo kati kati ya Ujerumani, Roland Koch, ametangaza kujiuzulu. Uamuzi wa mwanasiasa huyo, mwenye umri wa miaka 52, umekuja ghafla kwa watu wengi! Kwani yeye ni miongoni mwa viongozi muhimu wa chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel.

Wahariri wa magazeti karibu yote ya Ujerumani wanatoa maoni yao juu ya uamuzi wa mwanasiasa huyo mhafidhina.

Mhariri wa gazeti la Oldenburgische Volkszeitung anasema kujiondoa kutoka kwenye ulingo wa siasa kwa waziri Mkuu Roland Koch ni sawa na kukatikiwa na kamba kwa chama chake cha CDU na kwa siasa za Ujerumani kwa jumla. Kwani waziri Mkuu huyo ni mtu mwenye ujuzi mkubwa wa mambo ya fedha.

Gazeti la Nordwest linasema vyama vya kihafidhina vinampoteza mwanasiasa ambae katika upande mmoja ni machachari, lakini katika upande mwingine ni mwanasiasa kabambe. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa kuondoka kwa mwanasiasa huyo ni pigo kwa chama chake ingawa kwa tathmini za harakaharaka kuondoka kwake ni hatua ya faraja kwa mwenyekiti wa chama chake, Kansela Merkel, ambae ni mpinzani wake. Mhariri wa gazeti la Nordwest anasema ni kweli kwamba Roland Koch wakati mwingine alisababisha mfarakano ndani ya chama, chake lakini mwanasiasa huyo pia aliweza kuzivutia sauti zenye uzito katika upande wa chama chake. Mhariri huyo anasema mtu hahitaji kuwa nabii ili kuweza kutabiri kwamba vyama vya kihafidhina vitamkumbuka sana katika uchaguzi ujao.

Mtazamo huo unasisitizwa pia na gazeti la Hessische -Niedersächsiche Allgemeine kwa kusema kwamba ni jambo la kusikitisha kuwa Roland Koch ameamua kujitoa katika siasa wakati ambapo nchi inamhitaji.

Na mhariri wa Sächsiche Zeitung anasema wanasiasa kama Roland Koch hutokea kwa nadra,kwani yeye ni mtu asiyetumia kauli za mafumbo!
Mhariri huyo anasema Koch alipasua wazi, palipobidi kutetea msimamo wake. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kwamba mafanikio ya mwanasiasa yanapimwa kutokana na yale anayoyatekeleza. Msimamo wake unatambulika kutokana na maslahi anayoyapigania- na kwa ajili ya nani anayapigania maslahi hayo.

Gazeti la Sächische linasema na sasa Roland Koch ameamua kwenda katika mambo ya uchumi. Hakika huko ndiko kwenye wateja wake.Na huko ndiko hasa kunakomfaa.

Gazeti la Neue Osnabrücker linaunga mkono tathmini hiyo kwa kueleza kuwa waziri Mkuu Koch anastahili heshima kwa kuamua kujing'atua. Hata hivyo, jambo moja ni wazi: mwanasiasa huyo alifikia ukingoni katika medani ya siasa. Chama chake cha CDU hakina nguvu tena kama hapo awali katika jimbo lake la Hesse. Na wala hakuwa na uwezekano wa kupanda ngazi kisiasa, na kwa hiyo uamuzi wake wa kwenda katika sekta ya uchumi ni mbadala wa kufaa.

Mwandishi /Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Miraji Othman