1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya mashambulio ya Karachi

Abdu Said Mtullya10 Juni 2014

Pamoja na masuala mengine wahariri leo wanatoa maoni juu ya mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika kwenye uwanja wa ndege nchini Pakistan, Rais mpya wa Israel na juu ya Juncker

https://p.dw.com/p/1CFKp
Uwanja wa ndege wa Karachi baada ya kushambuliwa na magaidi
Uwanja wa ndege wa Karachi baada ya kushambuliwa na magaidiPicha: Reuters

Gazeti la "Nordwest" linayazungumzia mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika kwenye uwanja wa ndege wa Karachi nchini Pakistan.

Mwishoni mwa wiki iliyopita raia wapatao 30 na maafisa wa usalama waliuliwa na wapiganaji wa Taliban kwenye uwanja huo.Na leo zimepatikana habari kwamba wapinagaji wa Taliban walijaribu kulishambulia jengo la karibu na uwanja huo wa ndege. Juu ya kadhia hizo,mhariri wa gazeti la "Nordwest" anasema kuwa nguvu za Taliban bado hazijavunjika. Badala yake zinazidi kuwa kubwa ,licha ya kuwapo majeshi ya nchi za magharibi nchini Afghanistan na licha ya mshambulio yanayofanywa na ndege zisizokuwa na rubani.

Mashambulio yaliyofanyika kwenye uwanja wa ndege wa Karachi yanathibitisha jinsi Pakistan ilivyozidiwa nguvu.Mhariri wa gazeti la "Nordwest "pia anasema hujuma hiyo inaonyesha kwamba haina maana yoyote kufanya mazungumzo na magaidi.

Israel yachagua Rais mpya

Bunge la Israel leo linapiga kura kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo,atakaeichukua nafasi ya Shimon Peres anaetarajia kujiweka kando ya shughuli za siasa mwezi ujao. Mhariri wa gazeti la "Saarbrücker" anatoa maoni yake kwa kusema kwamba Shimon Peres ambae ni mwasisi wa mwisho wa Israel anaewaaga watu wake baada ya kuwatumikia kwa muda wa miaka mingi.

Peres anaukabidhi usukani kwa rika la pili la Israel.Lakini sivyo ambavyo alitumai. Katika muda wa zaidi ya miaka 60 aliyoitumikia nchi yake, Peres hakulifikia lengo la kuleta suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati .Haidhuru,ni nani atakaechaguliwa kuchukua nafasi yake,miongoni mwa wanasiasa wa Israel hakuna mwenye haiba,ujasiri na uwezo wa kuona mbali.

Juncker akabiliwa na upinzani wa Cameron

Jee nani atakuwa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya? Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linajibu swali hilo kwa kutilia maanani kwamba mjumbe wa vyama vya wahafidhina Jean Claude Juncker alipata kura nyingi katika uchaguzi,lakini viongozi muhimu kama Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron wanampinga mjumbe huyo.Huo ni mtihani mkubwa kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,anaeegemea upande wa Juncker. Na katika maoni yake gazeti la "Rhein Neckar" linashauri uchaguzi wa bunge la Ulaya ufanyike tena, kwa sababu wanachokifanya wanasiasa sasa ni kuwahadaa wapiga kura.

Mashindano ya kombe la dunia

Gazeti la "Bild" linayazungumzia mashindano ya kombe la Dunia nchini Brazil.

Gazeti hilo linayazingatia mambo mawili: kwanza wananchi wa Brazil wanafanya maandamano ya kuyapinga mashindano hayo.Siyo kwa sababu ati wanayachukia.Lakini kwa sababu wanauliza kwa nini gharama za ujenzi wa viwanja ziwe kubwa kuliko fedha zilizotumiwa na Ujerumani na Afrika Kusini kwa pamoja kwa ajili ya mashindano kama hayo? Na pili mashindano hayo yanafanyika katika muktadha wa kashfa kubwa ya rushwa kuhusu Katar kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka wa 2022.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman