1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI JUU YA MGOGORO WA MADENI

Abdu Said Mtullya10 Oktoba 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya mkutano wa Merkel na Sarkozy.

https://p.dw.com/p/12oz3
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Picha: dapd

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Sarkozy wa Ufaransa wamekutana mjini Berlin kuzijadili njia za kuukabili mgogoro mkubwa wa madeni ya Ugiriki.

Juu ya mkutano huo mhariri wa gazeti la Nordwest anasema hatari ya Ugiriki kushindwa kuyalipa madeni yake inazidi kukaribia. Lakini ili kuyaepusha mabenki, na hasa ya Ufaransa na athari za hatari hiyo, serikali za Ulaya pamoja na taasisi zinazohusika, zinachelewesha muda

Mhariri wa Nordwest anaeleza; kwanza nchi zote zinapaswa kuzikubali hatua zote zinazohusu mfuko wa kuziokolea nchi zenye madeni, na hatua ya pili itakuwa kuisamehe Ugiriki madeni yake na kuyaunga mkono mabenki. Lakini mhariri huyo anatilia maanani kwamba kwa mara nyingine mlipa kodi ndiye atakaelibeba zigo!

Mhariri wa gazeti la Nordwest anauliza, jee kutakuwa na malipo gani katika kuisamehe Ugiriki madeni yake? Mhariri huyo anajijibu mwenyewe kwa kusema kwamba Ugiriki itapaswa kujiondoa katoka Umoja wa Sarafu ya Euro. Na baadhi ya mabenki yatapaswa kutaifishwa. Anasema bila ya kuweka shubiri hiyo mtoto hataliacha titi.!

Gazeti la Mitteldeutsche pia linauzungumzia mkutano wa Kansela Merkel wa Ujerumani na Rais Sarkozy wa Ufaransa kwa kuitilia maanani dhima ya mabenki katika mgogoro wa madeni. Mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche anaeleza kwamba Mabenki yaliyochuma faida kubwa kutokana na dhamana za serikali ya Ugiriki sasa pia yanapaswa kushiriki katika kuubeba mzigo wa hasara vilevile.

Mhariri wa Nürnberger Zeitung anatoa maoni yake juu ya misaada ya serikali kwa mabenki. Anasena kuwa mabenki yana haki ya kuitumia kila fursa ili kujipatia faida. Lakini mhariri huyo anayaonya mabenki kwa kusema yasicheze patapotea kwa kutumai kwamba athari zake hazitaikumba jamii. Watu nchini Marekani sasa wamechachamaa dhidi ya ulariba wa mabenki. Mhariri wa Nürnberger anasema nchini Ujerumani vile vile hisia za watu zinapanda. Kwa hiyo msaada wowote wa mabilioni utakaotolewa kwa ajili ya mabenki lazima uandamane na masharti magumu.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/- Josephat Charo