1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Misri na Thomas Lubanga

Abdu Said Mtullya11 Julai 2012

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mvutano wa mamlaka nchini Misri na juu ya hukumu iliyotolewa kwa Thomas Lubanga

https://p.dw.com/p/15VHQ
Rais Muhammed Mursi wa Misri
Rais Muhammed Mursi wa MisriPicha: dapd

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya uamuzi wa mahakama Kuu ya katiba ya Ujerumani juu ya mfuko wa uokozi.

Juu ya Misri gazeti la"Weser Kurier" linasema Rais Mursi anafuata njia ya mvutano siyo tu dhidi ya Baraza la Kijeshi, bali pia na Mahakama Kuu ya Katiba. Rais huyo alitoa amri ya kuubatilisha uamuzi wa Mahakama hiyo wa kulivunja bunge. Lakini kwa kuchukua hatua hiyo, hata yeye mwenyewe hawezi kuamini kwamba mahakimu watakubali hukumu yao ifutike.

Gazeti la "Weser Kurier" linakumbusha kauli iliyotolewa na Jaji mkuu,kwamba hakuna mwananchi anayesimama juu ya sheria. Yumkini Rais mpya wa Misri hajalielewa hilo.

Naye mhariri wa "Frankfurter Rundschau" anasema katika maoni yake juu ya mvutano wa nchini Misri: "Dhamira ya Rais Mursi siyo tu ni kukabiliana na Baraza la kijeshi. Anachotaka kufanya ni kulipa fadhila. Jamaa zake wa Udugu wa Kiislamu walimsaidia katika kampeni ya uchaguzi. Kwa hivyo kuvunjwa kwa bunge maana yake ni kwamba wameyapoteza mamlaka.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" linasema mvutano wa mamlaka nchini Misri ni hatua ya hatari. Na linaeleza kuwa yanayotokea nchini Misri si mambo ya kufurahisha, hasa mtu akitambua kwamba nchi hiyo ni muhimu katika kuhimiza mchakato wa kuleta demokrasia katika Mashariki ya kati. Kwa sasa haijulikani ni nani hasa anashika hatamu za uongozi nchini Misri.

Mbabe wa kivita Thomas Lubanga amehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwatumia watoto kama askari vitani. Lakini gazeti la "Märkische Oderzeitung" linahoji katika maoni yake kwamba hukumu hiyo haijawatuliza watu. Kwa sababu. baada ya miaka minane atakuwa mtu huru, licha ya kutenda uhalifu wa kivita. Na mashtaka mengine hayakufikishwa mahakamani. Ni vizuri kwamba amehukumiwa, lakini mambo yangekuwa mazuri zaidi ikiwa waliotendewa uhalifu watalipwa fidia.

Waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, ameitaka Mahakama Kuu ya Katiba ya Ujerumani itoe uamuzi wa haraka juu ya mfuko wa uokozi. Lakini Mahakama hiyo bado haijaitaja tarehe ya kutoa uamuzi. Gazeti la "Der neue Tag" limetoa maoni kwa kusema kwamba mambo mengi muhimu yanahusika katika uamuzi huo. Mustakabali wa Ulaya na wa sarafu ya Euro. Muhimu siyo kusema ndio au hapana. Muhimu ni kuona ni kwa kiasi gani sheria zilizopo,zinaweza kuipeleka Ulaya mbele.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo