1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu amlaumu "Mufti" kwa maangamizi ya wayahudi

22 Oktoba 2015

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya kauli ya Waziri Mkuu wa Israel,Benjamin Netanyahu juu ya maangamizi ya wayahudi na pia juu ya mgogoro wa Syria

https://p.dw.com/p/1GsX7
Picha: Getty Images/C. Koall

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema inavyoelekea maji yameshamfika utosini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ,vinginevyo asingelijaribu kumhusisha aliekuwa kiongozi wa dini wa Wapalestina wa mwaka wa 1941 na yale yanayotokea sasa katika Mashariki ya Kati.

Mhariri wa gazeti la "Thüringer Landeszeitung" anasema ni kichekesho kikubwa kwa Waziri Mkuu Netanyahu anaefanya ziara ya kikazi nchini Ujerumani kumlaumu kiongozi huyo wa dini kwa maangamizi ya wayahudi ili kuyahalalisha yale wanayofanyiwa Wapalestina kwa muda wa miaka mingi.

Waziri Mkuu wa Israel alisema Jumanne iliyopita kwamba aliekuwa Kiongozi Mkuu wa Waislamu katika mji wa Jerusalem alimshawishi Fashisti Hitler kuwaangamiza wayahudi. Hata hivyo gazeti la "Straubinger Tagblatt" kwa upande wake linayazungumzia madai ya Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas kwamba wazayoni ndiyo wa kulaumiwa kwa maangamizi ya wayahudi.

Mhariri wa gazeti hilo anasema huo ni upuuzi wa kiwango cha juu kabisa.Lakini amesema hayo yanaakisi mazingira ya mvutano kwenye mazungumzo baina ya Waisraeli na Wapalestina.

Putin na al- Assad wakutana

Gazeti la "Berliner " linauzingatia mkutano baina ya Rais wa Urusi,Vladimir Putin na Syria Bashar al-Assad- Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba,nje ya mipaka ya Umoja wa Kisoviet, hakuna sehemu yoyote dunia ambako Urusi ilikuwa na ushawishi mkubwa kama nchini Syria.

Russland Syrien Assad bei Putin
Picha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Druzhinin

Mhariri wa "Berliner" anasema,kwa mtazamo wa Urusi, Syria ndiyo nchi pekee duniani ambayo, Urusi inaweza kuitumia ili kukwepa hali ya kutengwa na Marekani.

Mhariri huyo anaeleza kuwa Marekani ilikuwa na uhakika kwamba hapakuwa na haja ya kuishikirisha Urusi katika mgogoro wa Syria au kuhusu Iran.Gazeti la "Berliner" linasema Urusi yenyewe imejibebesha kazi ya kuvuruga amani.

Pegida ni hatari

Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche" anayatupia macho masuala ya ndani ya Ujerumani kuhusiana na harakati za kundi la watu wanaopinga kusilimishwa kwa bara la Ulaya-Pegida .Mhariri huyo anatilia maanani kwamba kundi la Pegida linazidi kuwa la siasa kali.

Hata hiyvo anasema siyo kila mtu anaeshiriki katika maandamano ya Pegida ni mtu anaefuata itikadi kali za mrengo wa kulia. Mhariri huyo anatambua kwamba watu wana hofu nchini Ujerumani kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi.

Hata hiyvo anasema miongoni mwa waandamanaji wa Pegida walikuwapo wale waliobeba kitu kilichomithilisha kitanzi kilichokuwa na majina ya viongozi- maana yake kwamba viongozi hao wanyongwe kwa sababu ya kuwatetea wakimbizi.

Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche" pia anatilia maanani katika maoni yake kwamba waandishi habari walishambuliwa na watu wa Pegida. Anasema hiyo ni hatari inayopaswa kukabiliwa kwa uthabiti wote. Ikiwa hatua hazitachukuliwa na dola, jamii itavunjika nguvu wakati Pegida inaendelea kustawi!

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Hamidou Oummilkheir