1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Papa Francis na juu ya Cyprus

Abdu Said Mtullya19 Machi 2013

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya Baba Mtakatifu Francis wa kwanza na juu ya Cyprus

https://p.dw.com/p/1802M
Baba Mtakatifu Francis wa kwanza akimbariki mtoto
Baba Mtakatifu Francis wa kwanza akimbariki mtotoPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la"Die Badische Zeitung" linasema katika maoni yake juu ya Baba Mtakatifu Francis wa kwanza kwamba yeye anatafautiana na Papa wapo hapo awali katika kuwasiliana na waumini.Mhariri wa gazeti hilo anasema Kiongozi huyo mpya wa Kanisa Katoliki siyo mtu anaeweka mbele sana nadharia za theolojia. Papa huyo kutoka Argentina Jorge Mario Bergoglio analijua jukumu lake tokea siku nyingi.Na kwa kulichagua jina la Francis wa Assis amejiwekea vipimo vya juu katika kazi yake.

Gazeti la "Neue Osnabrücker" linasema Papa Francis wa kwanza,ameingiza mtindo mpya na njia mpya ya mawasiliano katika Vatican.Ni mchangamfu na anazungumza kwa ufasaha .Ameonyesha kuwa mtu mwenye mafungamano na mazingira yake halisi. Mhariri wa gazeti la"Neue Osnabrücker"anatilia maanani kwamba Papa Francis wa kwanza anayazungumzia masuala yanayowagusa watu duniani,kama vile juu ya umasikini. Na vile vile anahubiri juu ya maadili ya msamaha.

Gazeti la "Der neue Tag"linatoa maoni juu ya mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuiokoa Cyprus. Lakini gazeti hilo linasema mpango huo umeivunja imani ya watu kama pigo la radi. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa hali hiyo imesababishwa na hatua ya kuwatoza kodi wananchi walioziweka fedha zao benki ikiwa pamoja na wale wenye akiba ndogo. Yumkini serikali itawatoza kodi wale wenye akiba inayozidi Euro,20,000 lakini ukweli ni kwamba uamuzi huo unaweza kusababisha athari kubwa .

Mhariri wa "Leipziger Volkszeitung" anasema uamuzi wa kuwatoza kodi watu walioweka fedha zao benki unawaathiri zaidi hasa wale ambao hawakusababisha mgogoro wa mabenki katika kisiwa cha Cyprus, yaani watu wa kawaida kama vile wastaafu na wafanyabiashara waadilifu. Kodi hiyo-yaani kutaifisha fedha za wananchi ni ishara ya hatari.Uhakika uliokuwapo barani Ulaya wa kuzilinda fedha za watu kwenye benki sasa umeanza kupoteza mashiko.Watu barani Ulaya sasa wakae wakijua kwamba wakati wowote akiba zao zinaweza kuchukuliwa.

Naye mhariri wa gazeti la "Heilbronner Stimme" anakubaliana na tahadhari hiyo kwa kusema kwamba habari kutoka Nicosia zinawatia wasi wasi watu walioweka fedha zao benki. Sasa kila mtu anajiuliza jee nini kinaweza kuwa salama tena?

Mhariri huyo anasema Ili kuwatuliza watu,viongozi wa Umoja wa Ulaya watapaswa kuwahikishia watu hao kwamba hatua iliyochukuliwa nchini Cyprus ni ya mara moja tu na kwamba imechukuliwa kutokana na mazingira maalumu.

Mhariri wa gazeti la"Kieler Nachrichten"anawashauri viongozi wa Umoja wa Ulaya waiachie Cyprus iyatatue matatizo yake yenyewe. Mhariri huyo anawataka viongozi wa Umoja wa Ulaya waachane na lugha ya mafumbo wanapouzungumzia mgogoro wa madeni barani Ulaya.Umoja wa Ulaya siyo chama cha sadaka.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman