1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magaidi wa Daesh wanafurahia mvutano

5 Januari 2016

Wahariri wanatahadharisha kwamba, mvutano baina ya Saudi Arabia na Iran unaweza kuudhoofisha mfungamano dhidi ya magaidi wanaoitwa dola la kiislamu. Abdu Mtullya

https://p.dw.com/p/1HY50
Maandamano dhidi ya Saudi Arabia
Picha: Reuters/T. Melville

Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya hatua iliyochukuliwa na Denmark ya kuufunga mpaka wake na Ujerumani ili kudhitibi wakimbizi

Gazeti la "Reutlinger General Anziger"linatilia maanani kushtadi kwa mvutano baina ya Saudi Arabia na Iran baada ya Saudi Arabia kuwanyonga watu zaidi ya 40 ikiwa pamoja na kiongozi wa Kishia Nimr - al- Nimr. Mhariri wa gazeti hilo anasema kwa kuanzisha mvutano na Iran, Saudi Arabia inacheza mchezo wa hatari. Mhariri huyo anasema msimamo wa Saudi Arabia unazipalilia mbegu za magaidi wanaoitwa dola la kiilsmu .

Saudi Arabia yaugawanya mfungamano dhidi ya magaidi

Mhariri wa "Reutlinger General Anzeiger" ameandika kwamba, wakati magaidi wa IS wamebanwa, Saudi Arabia inaugawa mfungamano dhidi ya watu hao. Mhariri wa gazeti la "Rhein-Necker" anasema ikiwa Saudi Arabia itatengwa katika Mashariki ya Kati, nchi hiyo itakuwamo katika hatari ya magaidi wenye itikadi kali.

Gazeti la "Nurnberger Nachrichten" linailaumu Marekani juu ya yale yanayotokea katika Mashariki ya Kati. Linasema mkakati wa Marekani wa kudhibiti mamlaka, umezitumbukiza Irak na Syria katika vurumai na hivyo kusababisha ujio wa magaidi wanaoitwa dola la kiilsamu, na katika mkakati huo Saudi Arabia ni mshirika alieridhia. Lakini inaonekana kana kwamba Marekani imepanda mchongoma na sasa kushuka ndio ngoma.

Wapinga kunyongwa kwa kiongozi wa Kishia Nimr Al-Nimr
Wapinga kunyongwa kwa kiongozi wa Kishia Nimr Al-NimrPicha: Reuters/T. Al-Sudani

Mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten" anaeleza kuwa,katika mchezo huo wa kisiasa, Ujerumani inaathirika zaidi kuliko Marekani ambayo mpaka sasa imechukua wakimbizi wachache tu. Pana haja ya kuambiana ukweli!

Gazeti la "Neue Ruhr linaelezea wasiwasi juu ya mgogoro wa nchini Syria, endapo mgogoro huo, sasa utaweza kutatuliwa, katika muktadha wa mvutano baina ya Saudi Arabia na Iran. Gazeti hilo linaeleza kwmba baada ya dalili za kukaribiana, zilizoonekana kwenye mazungumzo ya mjini Vienna, baina ya Saudi Arabia na Iran, kwa lengo la kutafuta suluhisho la Syria, sasa mambo yameenda mrama.

Matokeo yake ni maafa kwa watu wa Syria. Hatua ya Saudi Arabia ya kumnyonga kiongozi wa Kishia imewapa magaidi wa " IS" zana zaidi.

Gazeti la "Emder " linatoa maoni juu ya uamuzi wa Denmark wa kuufunga mpaka wake na Ujerumani ili kuwadhibiti wakimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema ingawa hatua hiyo ni ya muda, inatoa ujumbe ulio wazi kabisa. Kwamba enzi ya mipaka wazi barani Ulaya imeisha. Na hata moyo wa kiulaya juu ya uhuru umo katika hatari ya kuzimika.Ukweli ni kwamba nchi nyingine nazo zitaufuata mfano wa Denmark.!

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri:Josephat Charo