1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jee Papa Francis ataungwa mkono?

Admin.WagnerD2 Septemba 2015

Wahariri wanatoa maoni juu ya uamuzi wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis wa kuwaruhusu makasisi kutoa msamaha kwa wanawake waliotoa ujauzito

https://p.dw.com/p/1GQ0L
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Reuters/G. Sposito

Mhariri wa gazeti la "Badische" anasema Papa Francis anajua vizuri kwamba hatua aliyoichukua inahitaji uangalifu .Anatembea katika njia yenye utelezi. Mhariri huyo anasema wakati Baba Mtakatifu anaamini kuwa anajaribu kuleta mageuzi,wapinzani wake wanasema analolifanya ni jambo la kushtusha.

Gazeti la "Badische" linatilia maanani kwamba makasisi wenye moyo wa kuleta mageuzi watakuwa na kazi ngumu. Naye mhariri wa gazeti la Südwest Presse" anayo mashaka iwapo uamuzi wa Baba Mtakatifu Francis utaungwa mkono na maaskofu wengi.

Mhariri huyo anaeleza kwamba Baba Mtakatifu ameutoa wakati mwafaka,uamuzi wake juu ya kuwaruhusu makasisi kutoa msamaha kwa wanawake waliotoa ujauzito. Ameutoa uamuzi huo wakati wa kuuwasilisha ujumbe wa mwaka mtukufu kwa wakristo,unaoanzia tarehe 8 mwezi wa Desemba. Baba mtakatifu anaionyesha njia ya kuifuata kabla ya kufanyika kwa baraza la maaskofu mnamo mwezi wa Oktoba.

Vipi kanisa litahusiana na watu walioa au waliolewa tena baada ya ndoa zao kuvunjika hapo awali, na vipi kanisa litahusiana na watu wanaofanya mapenzi ya jinsia sawa. Lakini swali ni iwapo Baba Mtakatifu ataungwa mkono na Maaskofu wengi.

Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anasema uamuzi wa kiongozi wa Kanisa Katoliki unaonyesha kwamba hakuna jambo lisiloweza kusamehewa duniani. Kila kitu kinaweza kuanzishwa upya.

Amani imo mashakani nchini Ukraine

Gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger " linauzumgzia mchakato wa amani wenye mashaka nchini Ukraine. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba mtu anaweza kumtahadharisha Rais Poroshenko na wafuasi wake au anaweza kujaribu kuwashinikiza.

Ukraine Unabhängigkeitstag - Petro Poroschenko
Rais wa Ukraine Petro PoroschenkoPicha: Reuters/G. Garanich

Lakini mhariri anasena mtu hawezi kuyatekeleza hayo kwa kuacha kuiunga mkono Ukraine, kiuchumi na kisiasa.Sababu ni kwamba Ukraine siyo mvamizi bali ni mvamiwa.Ukraine siyo iliyopekela askari wake vitani mnamo mwezi wa Aprili,bali ni Urusi. Sasa ni juu ya Ulaya kuamua iwapo mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Minsk juu ya kuleta amani nchini Ukraine bado unaendelea kutekelezwa.

Gazeti la "Mitteldeutsche" linatilia maanani kwamba Rais Poroshenko anataka kuyapa majimbo ya mashariki mwa Ukraine mamlaka ya ndani kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini mjini Minsk.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema Rais huyo anashutumiwa na wapinzani na wale wenye itikadi kali wamerusha gurudeni kwenye maandamano.Mhariri huyo anasema matukio kama hayo,yanamnufaisha mtu mmoja tu,naye ni bwana Vladimir Putin wa Urusi.

Mwandishi: Abdu Mtullya/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef