1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya uchaguzi, Bulgaria na Pakistan

Abdu Said Mtullya14 Mei 2013

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya chaguzi za Pakistan na Bulgaria kutilia maanani kauli za viongozi wa Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/18XNs
Nawaz Sharif arejea tena katika kitovu cha siasa nchini Pakistan
Nawaz Sharif arejea tena katika kitovu cha siasa nchini PakistanPicha: Arif Ali/AFP/Getty Images

Juu ya uchaguzi wa nchini Pakistan gazeti la "Landeszeitung Lüneburg" linaitilia maanani kauli ya Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton kwamba uchaguzi huo ni ushindi wa kihistoria kwa demokrasia ya nchi hiyo.Lakini mhariri wa "Landeszeitung Lüneburg" anasema pana hatari, huenda pongezi hizo zikauficha udhalimu.

Anasema kwanza yapasa kutambua kwamba mshindi wa uchaguzi Nawaz Sharif   anapakatana na Taliban.Pili anaiegemea Saudi Arabia. Na tatu udini katika vyama vikuu ni jambo linalosababisha wasi wasi.

Gazeti la "Neue Osnabrücker" linautupia macho uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Bulgaria, yaani nchi masikini kabisa katika Umoja wa Ulaya.Mhariri wa gazeti hilo anasema mambo ni mabaya kwa nchi hiyo.

Anaeleza kuwa Bulgaria inakabiliwa na matatizo mengi makubwa, ikiwa pamoja na  kiwango kikubwa sana cha ukosefu wa ajira.Bei za mahitaji ya kila siku zinazidi kupanda na mifumo ya elimu na afya ni taabani. Uchaguzi uliofanyika ulikuwa na lengo la kuwapa watu wa nchi hiyo mwelekeo mzuri wa kisiasa na serikali yenye uwezo wa kupitisha maamuzi. Lakini hata nusu ya malengo hayo haikufikiwa. Bulgaria imo katika hatari ya kukwama tena kisiasa, hali inayoweza kusababisha   ghasia miongoni mwa wananchi.

Gazeti la "die tageszeitung" linasema kuwa matokeo ya uchaguzi nchini Bulgaria ni pigo kubwa kwa demokrasia, kwani zaidi ya nusu ya wapiga kura hawakuitumia haki ya kushiriki katika uchaguzi. Naye mhariri wa "Frankfurter Rundschau"anasema kilichoonekana katika uchaguzi wa nchini Bulgaria ni hali ya kukata tamaa miongoni  mwa wananchi.

Mhariri huyo anaeleza kwamba wapinzani waliomtimua Waziri Mkuu wa nchi  hiyo,Borisov miezi mitatu iliyopita bado hawajashindwa.Katika kipindi kifupi kabla ya uchaguzi kufanyika wapinzani hao hawakuweza kujitokeza na wajumbe wao.Ndiyo kusema bado wana dukuduku linaloweza kulipuka wakati wowote.Mhariri wa "Frankfurter Rundschau" anasema ikiwa kambi za wahafidhina na wasoshalisti zitashindwa kuyafanya maisha ya watu masikini wa Bulgaria kuwa bora, nchi hiyo itakuwamo katika hatari ya kuingia katika mikono ya watu wenye itikadi kali na ya wababaishaji.

Gazeti la "Süddeutsche" linaishauri Bulgaria iunde mseto wa kitaifa wa kuleta mageuzi.Linasema mahafidhina na wasoshalisti kwa kushrikiana na wataalamu   wanapaswa kuchukua hatua ya kijasiri ya kuwapa watu wa Bulgaria kile ambacho hasa wanakihitaji: utulivu wa kisasa,hali bora ya kiuchumi na kuundeleza mchakato  wa mageuzi ya kijamii. Mageuzi ya dhati ya kijamii ndiyo utakuwa msingi wa mustakabal imara wa Bulgaria.

Mwandishi:Mtullya  Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu