1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Ugiriki

Abdu Said Mtullya24 Julai 2012

Wahariri wa magazeti karibu wote leo wanazungumzia juu ya Ugiriki. Lakini pia wanatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria baada ya mawaziri wa Umoja wa Ulaya kukutana.

https://p.dw.com/p/15dtm
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Philipp Rösler
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Philipp RöslerPicha: picture-alliance/dpa

Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anauliza jee ni kwa muda gani nchi za Umoja wa sarafu ya Euro zitaendelea kuibeba Ugiriki? Shirika la Fedha la Kimataifa pamoja na Tume ya Umoja wa Ulaya zinasisitiza uaminifu kwa Ugiriki. Lakini masoko yameshakata tamaa juu ya Ugiriki.

Gazeti la "Leipziger Volks-stimme" pia linasema kwamba Ugiriki inakaribia kufilisika, na linaeleza kuwa Ugiriki sasa imekuwa shimo lisilokuwa na mwisho. Nchini Ujerumani na kwenye Shirika la fedha la Kimataifa watu wameanza kutambua kwamba haiwezekani tena kuepusha kusambaratika kwa Ugiriki. Mpaka sasa hakuna kilichofanyika nchini Ugiriki, kuukabili mzizi wa mgogoro.

Lakini mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten "anatahadharisha juu ya madhara ya kufilisika kwa Ugiriki. Mhariri huyo anasema kuwa ni sahihi kabisa kwa Ujerumani kukataa kutupa fedha katika shimo lisilokuwa na mwisho.Lakini kufiliska kwa Ugiriki na kujitoa kwenye Umoja wa sarafu ya Euro kunaweza kuwa hatua ya gharama kubwa kwa nchi nyingine za Umoja wa sarafu ya Euro.Kauli ya Waziri wa uchumi wa Ujerumani Rösler kuwa wakati wa Ugiriki kuondoka kwenye Umoja wa Euro ulishapita zamani ni sahili mno yaani nyepesi sana. Kauli hiyo imesababisha miyumbiko kwenye masoko ya fedha.

Naye mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten" anasena baadhi ya wanasiasa kama,Waziri wa uchumi wa Ujerumani wanachezea moto badala ya kuuzima. Mhariri wa gazeti hilo anawataka wanasiasa hao wapime uzito wa madhara yatakayotokea baada ya Ugiriki kutoka kwenye Umoja wa Euro.

Gazeti la "Saarbrücker linatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria na msimamo wa nchi za Umoja wa Ulaya. Linasema, Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya wameeleza wazi juu ya mauaji halaiki nchini Syria na wamemwambia Rais Assad kinachomsubiri; kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague, lakini mawaziri hao wanapaswa kujua kwamba maji ya moto hayaunguzi nyumba- kauli tupu hazitakomesha vita nchini Syria.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Abdul-Rahman