1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya uwanja wa ndege wa Berlin

Abdu Said Mtullya8 Januari 2013

Wahariri wanazungumzia juu ya mishkeli inayouandama mradi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Berlin na pia wanatoa maoni juu ya hali ya kisiasa nchini Venezuela

https://p.dw.com/p/17Fkv
Meya wa jiji la Berlin Klaus Wowereit (SPD) aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya kusimamia ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Berlin aamua kujiuzulu uenyekiti huo
Mwenyekiti wa bodi ya kusimamia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Berlin, Klaus Wowereit ajiuzuluPicha: picture-alliance/dpa

Mradi wa uwanja wa ndege wa Berlin umekuwa unaandamwa na mishkeli kadhaa.Uwanja huo mpya ,Willy Brandt ulipangwa kufunguliwa mnamo mwezi wa Oktoba. Lakini ufunguzi umeahirishwa kwa mara ya nne.Na jambo la kukera ni kwamba kila ufunguzi unapoahirishwa gharama nazo zinazidi kuongezeka.Makosa kadhaa ya kiufundi yamejitokeza katika mradi huo.Kutokana na hayo Mwenyekiti wa bodi ya kusimamia ujenzi wa uwanja huo,Meya wa jiji la Berlin,Klaus Wowereit amejiuzulu.

Gazeti la "Berliner Morgenpost" linasema " Meya wa jiji la Berlin Wowereit anapaswa kuyamaliza matatizo yanayoukabili mradi wa uwanja wa ndege mypa wa mjini Berlin. Lazima ahakikishe kwamba uwanja huo hatimaye unafunguliwa bila ya kujali ni lini.

Juu ya kujiuzulu kwa Meya Wowereit uenyeketi wa kusimamia ujenzi wa uwanja huo mhariri wa gazeti la "Braunschweiger"anaeleza kwamba ni wazi Mwenyekiti wa Bodi ya ujenzi wa uwanja hawezi kuzijua habari zote za kifundi juu ya ujenzi. Lakini anasema madhumuni ya kuwepo Mwenyekiti ni kuhakikisha kwamba shughuli za ujenzi zinasonga mbele. Lakini sasa Mwenyekiti huyo amejiuzulu,Hiyo haitoshi.

Lakini mhariri wa gazeti la "Lausitzer" anasema lazima awepo mtu wa kuchukua dhamana pale panapofanyika kosa. Mhariri huyo anaeleza: Baada ya ufunguzi wa uwanja kuahirishwa mara nne, na kusababisha gharama kubwa sana, ni wazi kwamba anaehusika hana budi ajiwajibishe, aondoke.Kutokana na kuruhusu uzembe,Wowereit ameligeuza jimbo lote kuwa kichekesho.Kwa kweli inatosha!

Gazeti la Donaukurier" linasema siyo tu,Mwenyekiti wa kusimamia ujenzi anaepaswa kuondoka ,bali pia Mkuu wa uwanja wa ndege,Rainer Schwarz ,hana budi afunge virago,kwa hiari yake,kabla ya kutimuliwa.Japo hatua hiyo pia haitamwepusha mlipa kodi kubeba gharama za ujenzi.

Venezuela:

Gazeti la "Die Welt" linatoa maoni juu ya hali ya kisiasa nchini Venezuela kwa kutilia maanani mchango wa Rais Chavez katika maendeleo ya nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anasema "Yatakuwa mawazo mafupi, kufikiria kwamba umaarufu wa Rais Chavez unatokana na fedha za mafuta tu. Kwani amefanikiwa kuwaridhisha mamilioni ya watu nchini mwake na kwingineko, na hasa wale wanaopunjika. Lakini matumizi yake ya fedha ni mabya,na sasa takriban, hakuna kampuni za watu binafsi,na pia amejenga tabia tegemezi miongoni mwa watu wake. Hakika hicho siyo kigezo cha kufaa kwa mustakabal wa Venezuela.

Mwandishi:Mtullya abdu.Deustche Zeitungen:

Mhariri:Saumu Yusuf