1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Zuma na Ngudjolo Chui

Abdu Said Mtullya19 Desemba 2012

Wahariri wanatoa maoni juu ya kuchaguliwa tena kwa Jacob Zuma kuwa Rais wa chama cha ANC na pia juu ya aliyekuwa mbabe wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Ngudjolo Chui

https://p.dw.com/p/175N4
Zuma achaguliwa tena kuwa Rais wa ANC
Zuma achaguliwa tena kuwa Rais wa ANCPicha: Stephane de Sakutin/AFP/Getty Images

Kuhusu kuchaguliwa tena kwa Jacob Zuma na hivyo kuendelea kuwa Rais wa chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, gazeti la "Süddeutsche" linasema licha ya mwanasiasa huyo kuchaguliwa kwa kishindo, Afrika Kusini imo katika mgogoro mkubwa. Mhariri wa gazeti hilo anasema sababu ya mgogoro huo ni kashfa na udhaifu uliomo katika uongozi wa Zuma. Gazeti linasema Afrika kusini ilikabiliwa na migomo iliyoandamana na umwagikaji wa damu. Hali hiyo ilisababisha hasara katika uzalishaji na kuiathiri sekta ya uchumi.


Gazeti la "Stuttgarter" linasema, chama cha ANC kinaweza kugawanyika katika siku za usoni kutokana na kushindwa kuzitimiza ahadi nyingi kilizozitoa kwa wafuasi wake.Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema mpaka sasa chama cha ANC bado kinaungwa mkono na mamilioni ya watu. Sababu ni kwamba kwa mamlioni ya waaafrika chama cha ANC kimeleta ukombozi. Lakini ahadi ambazo chama hicho kilizitoa kwa mamilioni ya wananchi bado hazijatekelezwa mpaka leo.

Watu wengi hawana ajira, na idadi yao inaongezeka,mfumo wa elimu kwa ajili ya waafrika una mapungufu. Mamilioni ya waafrika wanaendelea kuishi katika vitongoji vya masikini. Kwa hivyo kuchaguliwa tena kwa Zuma kukiongoza chama cha ANC, kunaweza kusababisha mpasuko ndani ya chama hicho.

"Mbabe wa kivita Ngudjolo Chui aachiwa"

Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague ICC jana ilimwachia huru ,aliekuwa mbabe wa kivita Ngudjolo Chui aliefikishwa mbele ya mahakama hiyo kujibu mashtaka ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Lakini hakupatikana na hatia.

Juu ya hukumu hiyo gazeti la "Neue Osnabrücker" linasema:"Jambo moja ni la uhakika: uhalifu ulifanyika katika kijiji cha Bogoro mashariki mwa Kongo. Watu waliuawa,wengine walichomwa moto wakati wakiwa hai, na wanawake walibakwa. Lakini Ngudjolo Chui hakupatikana na hatia ya mashtaka hayo" Gazeti la "Neue Osnabrücker " linasema hukumu hiyo inathibitisha kwamba Mahakama ya mjini The Hague, ICC inafanya kazi yake . Hatahivyo waendesha mashtaka wanayo haki ya kukata rufaa.

Mhariri wa "die tageszeitung" anakubaliana na mtazamo huo na anasema: Mahakimu wa ICC wamebainisha kwamba mashtaka yaliyomkabili Chui yalikuwa na mashaka-mashahidi wengi hawakuwa wazi katika kauli zao-walibabaika na hawakuaminika. Katika hali hiyo mshtakiwa hawezi kutiwa hatiani.Ni sahihi kabisa kwamba mahakimu wametoa haki pia kwa mbabe wa kivita.

Mwandishi: Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Mohammed Khelef