1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri kuhusu Serbia na uchaguzi nchini Marekani

Maja Dreyer5 Februari 2008

Katika uchaguzi wa Jumapili, Waserbia walimrefushia raisi wao Boris Tadic muda wake madarakani, japo kwa ushindi mdogo.

https://p.dw.com/p/D30G
Boris Tadic, rais wa Serbia
Boris Tadic, rais wa SerbiaPicha: AP
Umoja wa Ulaya sasa unapanga kuimarisha uhusiano wake na Serbia ukitarajia eneo la Kosovo kutangaza uhuru wake. Tusikie basi kwanza maoni ya mhariri wa "Süddeutsche Zeitung" kuhusu matokeo haya:

"Katika uchaguzi huu, Waserbia walitumia akili. Kwa kumchagua tena Boris Tadic walizuia matatizo mengi na kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura Waserbia walionyesha kwamba hawataki nchi yao itenganishwe kisiasa. Uchaguzi huu ulikuwa kama kura ya maoni ya kupinga utawala wa chama cha kizalendo ambacho kinakataa Umoja wa Ulaya na kinataka ushirikiano na Urusi."
Gazeti la "Kölnische Rundschau" linaangalia zaidi upande wa Umoja wa Ulaya na limeandika:
"Jibu la Umoja wa Ulaya kuhusu ushindi wa Boris Tadic ni faraja. Wakuu wote wa Umoja huu walimpongeza Tadic wakifurahi tu kwamba si lazima kuzungumza na kiongozi wa wazalendo wakali."
Na hatimaye kuhusu uchaguzi wa Serbia ni maoni ya gazeti la "Die Welt" ambalo linazingatia zaidi suala la Kosovo:
"Licha ya matokeo yake mazuri, uchaguzi huu wa rais unaonyesha jinsi jamii ya Serbia ilivyogawika kati ya wazalendo wanaotaka kushirikiana na Urusi na kuendelea na vita vya zamani kwa upande mmoja na wale wanaotaka Serbia ijiunge na Umoja wa Ulaya. Kwa hiyo Ulaya imefanya vizuri kuipatia Serbia matumaini ya kujiunga na Umoja huu ili kuishawishi ikubali uhuru wa Kosovo."
Mada nyingine muhimu kwenye kurasa za wahiri siku ya leo ni kiinyang'anyiro cha wagombea nafasi ya kutetea wadhifa wa urais nchini Marekani katika majimbo 24 ya Marekani. Bado haijulikano kama matokeo yake yataleta uamuzi nani atapigania urais kwa vyama viwili vikubwa. Hata hivyo, mhariri wa "Ostthüringer Zeitung" anasema:
"Bila ya kujali matokeo ya uchaguzi wa leo na pia bila ya kujali nani atakuwa raisi mpya, tayari leo tunaweza kusema: wagombea wanne wote ambao bado wana nafasi ya kushinda, kisiasa ni chaguo zuri kuliko lile la kabla ya uchaguzi wa mwaka 2004."
Na la mwisho ni gazeti la "Neue Ruhr/Neue Rhein" ambalo linaangalia zaidi upande wa Wademokrats na wagombea wao wawili Barack Obama na Hilary Clinton. Gazeti limeandika:

"Tofauti ya kisiasa kati ya wagombea hao wawili ni ndogo sana. Tena si suala la jinsia wala la rangi. Suala hasa ni ikiwa Wademokrats wanarudi kwenye enzi ya Clinton au kuelekea kizazi kipya."