1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri na ABDU MTULLYA

7 Februari 2007

Jumuiya ya wafanyakazi ya hapa nchini Ujerumani IG Metall imesema itadai nyongeza ya asilimia 6 nukta 5 katika mishahara ya wafanyakazi kwenye mazungumzo na waajiri yatakayofanyika mwezi aprili. Hilo ndilo suala linalozingatiwa na wahariri wa magazeti katika maoni yao leo.

https://p.dw.com/p/CHTm

Katika maoni yao wahariri pia wanazungumzia juu ya uamuzi wa mwanasiasa mashuhuri wa chama cha CDU bwana Friedrich Merz kujiweka kando na siasa .

Mhariri wa Gazeti la Die WESTFALENPOST anasema juu ya msimamo wa jumuiya ya wafanyakazi IG Metall kudai nyongeza ya asilimia 6 nukta 5 katika mishahara ya wafanyakazi kuwa hakika pana haja ya kuongeza mishahara hiyo kwa kutambua kwamba utaratibu wa mgawano umeathirika na kodi za juu, michango ya juu ya bima, na kutokana na kuondolewa nafuu za kodi ya kichwa.

Gazeti hilo linasema yote hayo yamechangia katika kuifanya mifuko ya watu ididimie.

Gazeti linaunga mkono dai la jumuiya ya wafanyakazi, kwa sababu linasema,nyongeza ya mishahara itaimarisha utashi wa ndani. Lakini mhariri anatahadharisha kuwa mzigo huo wa malipo lazima ufungwe vizuri ili kuweza kubebwa hata na viwanda visivyopata faida kubwa.

Mhariri wa gazeti la KÖLNER-STADT ANZEIGER , katika maoni yake anatoa mwito juu ya kuwapo busara baina ya waajiri na waajiriwa.

Anasema kuwa dai la kuongezwa asilimia 6 na nukta tano ni la juu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hivyo basi inaeleweka kuwa waajiri wanalalamika licha ya ukweli kwamba makubaliano yatakuwa chini ya kiwango hicho kama ilivyo desturi ya mapambano baina ya pande mbili hizo.

Lakini pia anawashauri wawakilishi wa wafanyakazi juu ya kutoivutia sana ngozi upande wao. Busara inapasa kuwa msingi wa mazungumzo na kuwa tayari kufikia usikizano.

Mhariri wa gazeti la SHWÄBISCHE ZEITUNG kutoka mji wa Leutkirch amewakariri watafiti wanaotabiri kuwa waajiri watakuwa tayari kuongeza mishahara kwa asilimia 4.

Mhariri huyo anatilia maanani kuwa vitabu vya makampuni vimejaa tenda pomoji na kwa hivyo mgomo litakuwa jambo la mwisho kabisa kujiombea. Lakini mhariri huyo pia anawatanabahisha wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kuwa uzito wa vyama hivyo unapungua, kwa hiyo nyongeza ya asilimia 4 haitakuwa haba.

Gazeti la mjini Berlin, BERLINER ZEITUNG nalo linasisitiza hoja hiyo hiyo . Linakumbusha kwamba hapo awali kulikuwa na nyongeza ya asilimia 3, sambamba na kitita cha mara moja. Lakini kitita hicho kinaweza kuongezwa ama kupunguzwa kwa kutegemea na hali ya biashara. Lakini safari hii wawakilishi wa vyama vya wafanya wamekataa utaratibu huo. Juu ya hayo mhariri anasema anatumai kuwa hiyo haikuwa kauli ya mwisho ya wawakilishi hao.

Wahariri leo pia wanatoa maoni yao juu ya uamuzi wa mwanasiasa mashuhuri wa chama cha CDU bwana Friedrich Merz kujibaidisha na siasa.

Juu ya hayo mhariri wa gazeti maaruf la mji wa Düsseldorf HANDELSBLATT anasema kuwa uamuzi wa bwana Merz kujiuzulu ni mwanzo wa mjadala uliokandamizwa muda mrefu ndani ya chama cha CDU juu ya sera za kijamii na kiuchumi za chama hicho kilichomo katika serikali ya mseto na chama cha SPD.