1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri na ABDU MTULLYA

6 Februari 2007

Katika maoni yao wahariri wa magazeti leo wanazungumzia juu ya uamuzi wa mahakamu kuu ya Ujerumani kuwakataza polisi kutumia soft ware za upelelezi ili kuchunguza kompyta za wananchi. Kufuatia uamuzi huo polisi hapa nchini hawataweza kuchunguza kompyuta ya mtuhumiwa bila ya mwenyewe kujua.

https://p.dw.com/p/CHTn

Mhariri wa gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE anaesema kuwa uamuzi uliotolewa na mahakama kuu ya mjini Karlsruhe haumaanishi kuwa utaratibu kama huo hauruhusiwi kabisa.

Bali ni lazima msingi wa sheria uwekwe utakaozingatia maslahi ya nchi.

Mhariri anasema haja ya kulinda data za wananchci asilani isiwe kizingiti katika juhudi za kupambana na wahalifu wakubwa. Pamoja na hayo nani anaweza kuamini kwa moyo wote kuwa pana usalama katika internet.

Mhariri wa gazeti la LANDSHUTTER ZEITUNG anatoa mwito juu ya kuwapo sheria mujarabu .Mhariri huyo anatilia maanani kwamba wahalifu wa kawaida, achilia mbali magaigi, wameshagundua kutumia mtandao wa kompyuta kwa malengo yao mbalimbali ya kihalifu. Mhariri anasema kutokana na uamuzi wa mahakama kuu kuwakataza polisi kutumia software za siri kuwafuatilia watuhumiwa wa uhalifu, sasa ni juu ya watunga sheria hapa nchini kutafuta suluhisho.Anasema hasa katika zama hizi za ugaidi, wa kimataifa litakuwa kosa kuwazuia walinda usalama kufanya kazi yao.

Naye mhariri wa gazeti ,la ALLGEMEINE ZETUNG MAINZ anasisitiza hayo hayo kwa kusema kuwa ni lazima itungwe sheria itakayoruhusu kuchunguza yanayofanyika katika mitandao ya kompyuta.

Kutokana na hatari ya ugaidi kushtadi duniani, na kutokana na baadhi ya wahalifu kuwa na ujuzi wa juu katika tekinolojia inahalisi kabisa kwa walinzi wa usalama kupewa nyenzo za kuweza kupambana na wahalifu hao .Lazima pawepo na sheria ya kuwaruhusu walinda usalama hao kufanya kazi yao.

Gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG linasema ,inaeleweka kuwa watetezi wa haki za raia wana wasiwasi juu ya kutokea mazingira mithili ya yale yaliyobashiriwa na mwandishi wa riwaya George Orwell ambapo kila nyanja ya jamii inamulikwa na vyombo vya usalama. Lakini mhariri huyo anakumbusha juu ya matendo ya kigaidi ambayo yangeliweza kuzuiliwa kwa kutumia utaalamu wa kisasa.

Akiunga mkono uamuzi wa mahakama kuu kupiga marufuku matumizi ya softaware za siri ili kuwachunguza wahalifu,mhariri wa gazeti la BADISCHE TAGBLATT anasema haifai kujidangaya kwani uchunguzi huo hautalekezwa kwa magaidi na waharibifu wa watoto tu ! Yeyote mwenye kompyuta nyumbani anaweza kutiwa katika mkumbo wa kuchuguzwa. Hivyo basi pana ulazima wa kutafakari vizuri zaidi juu ya sheria itakazoziwezesha idara za usalama kuingia ndani ya kompyuta za wananchi na kufanya upelelezi.