1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri na Abdu Mtullya

12 Oktoba 2006

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mkasa wa kusikitisha wa mtoto aliegunduliwa amekufa ndani ya friji.

https://p.dw.com/p/CHUi

Kwa mara nyingine watu wameshtushwa sana nchini Ujerumani baada ya kusikia habari juu ya maiti ya mtoto iliyogunduliwa ndani ya friji.!

Mtoto huyo aliekuwa na umri wa miaka 2 alikuwa analelewa na baba yake mwenye uraibu wa madawa ya kulevya.

Mkasa huo uliotokea katika mji wa Bremen umewashtusha sana watu hapa nchini hasa kwa kutambua kwamba idara inayohusika ilizembea katika wajibu wake.

Akitoa maoni yake juu ya kifo cha mtoto huyo mhariri wa gazeti la NEUE WESTFÄLLISCHE la mjini Bielefeld anasema kuwa hii si mara ya kwanza kwamba idara inayohusika kuzembea na kushindwa kutimiza wajibu wake katika kulinda maslahi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Naye mhariri wa gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG anakumbusha katika maoni yake kwamba baba wa mtoto huyo ni mlevi mkubwa—mtu huyo ana uraibu wa kutumia madawa ya kulevya kama heroini. Pamoja na hayo mtu huyo yupo chini ya uchunguzi kuhusiana na kifo cha mkewe. Lakini licha ya hayo yote, bwana huyo aliendelea kumlea mtoto huyo.

Idara ya vijana ndiyo ilikuwa na wajibu juu ya mtoto huyo, lakini kuanzia mwezi wa julai hakuna afisa yeyote kutoka idara hiyo aliemwona Kevin, hadi jana ambapo maiti yake iligunduliwa ndani ya friji!

Mhariri wa gazeti hilo anasema mkasa huo hauna mithili katika jinsi idara za serikali zinavyokiuka wajibu.

Katika maoni yake mhariri wa gazeti hilo amemkariri waziri mkuu wa jimbo la Bremen akisema, watoto wanapaswa kuwa na uhakika kwamba serikali yao inawalinda.

Mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE anasema mkasa wa mtoto huyo unasikitisha zaidi kwa sababu ni serikali iliyoshindwa kutimiza wajibu wake. Mhariri huyo anauliza vipi iliwezekena kwa mtoto huyo aliekuwa na umri wa miaka miwili kulelewa na mtu anaetumia madawa ya kulevya na ambae yupo chini ya uchunguzi juu ya madai kwamba alimwuua mkewe?

Gazeti hilo linakumbusha kwamba mama wa mtoto huyo pia alikuwa anatumia madawa ya kulevya,na kwamba idara ya vijana ilijua hayo. Kwa nini basi idara hiyo haikuchukua hatua , japo ndiyo iliyokuwa na wajibu juu ya malezi ya mtoto huyo?

Na mhariri wa gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG anasikitika zaidi kwa sababu anasema , kifo cha Kevin kingeliweza kuepushwa.