1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo6 Novemba 2007

Licha ya kukosolewa vikali na upinzani, chama cha SPD na muungano wa CDU-CSU, vinataka kuongeza marupurupu ya wabunge wanapohudhuria vikao vya bunge. Wakati huo huo vyama hivyo vinataka kupunguza malipo ya uzeeni. Mswada huo unatarajiwa kujadiliwa kwa mara ya kwanza bungeni Ijumaa ijayo. Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejishughulisha na swala hilo.

https://p.dw.com/p/C7l0

Tunaanza na gazeti la Kieler Nachrichten: Mhariri anasema hakuna wakati muafaka wa kuongeza malipo ya kuhudhuria vikao kwa wabunge. Karibu mijadala yote itakayozuka ili kujaribu kuzuia nyongeza ya malipo ya wabunge inafaa katika kila awamu ya uchumi na kipindi cha uchaguzi.

Anayetaka kupata nyongeza kubwa ya idadi ya kura za wananchi, anatakiwa aachane kabisa na mradi huo. Shinikizo la wazi tayari limesababisha ongezeko la malipo katika miaka iliyopita kushindwa kutimia na wabunge wamekuwa wakijiepusha mbali na mishahara ya mahakimu wa Ujerumani, ambayo bado wanataka kuilewa vizuri.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema mjadala kuhusu nyongeza ya marupuruu kwa wabunge kwa kuhudhiria vikao unapunguza nafasi ya chama chochote kuweza kushinda uchaguzi. Ikiwa pendekezo hilo litapitishwa kila mbunge atapokea kiasi cha euro 7,700 kila mwezi pamoja na kiwango cha euro 3,700 ambacho hakitozwi kodi. Hayo si malipo ya kifahari ikizingatiwa jukumu kubwa walilonalo wabunge na matumizi yao ya hivi sasa.

Hata hivyo wakati huo huo ipo haja ya kuufanyia marekebisho mfumo wa malipo ya uzeeni ambao umekuwepo kwa vipindi viwili sasa vya bunge. Ikiwa vyama vya CDU na SPD vitafaulu kupitisha nyongeza ya malipo ya wabunge wanapohudhuria vikao, kwa mtazamo wa bunge utakuwa ni ushindi mkubwa.

Mhariri wa gazeti la Ostthüringer la mjini Gera anasema swala la ngongeza ya marupurupu kwa wabunge halina haja ya kufafanuliwa zaidi. Lakini sehemu ya pili ya mswada uliotayarishwa na chama cha SPD na CDU utakaowasilishwa bungeni Ijumaa ijayo, unazusha maswali, hususan pendekezo la kupunguza malipo ya uzeeni ya wabunge.

Mswada huo una upungufu ambao unaufanya ushukiwe. Mabadiliko halisi yangechukua muelekeo mwingine unaoonyesha ari ya kutaka kufanya mageuzi ya kweli. Hakuna anayewaonea wivu wanasiasa kwa kulipwa mishahara mikubwa, lakini ili mradi msaada wa uzeeni utabakia kutolewa, basi wabunge hawatatakiwa kushangaa wakati kila mmoja wao atakapolazimika kutangaza hadharani nyongeza ya marupurupu waliyopewa kihalali kwa sababu ya tuhuma.

Tukimalizia na gazeti la Märkische Allgemeine kutoka Potsdam, mhariri anasema vyama vya SPD na CDU vimeungana katika swala la kutaka kuongeza malipo kwa wabunge na kwa nguvu.

Mhariri wa gazeti hilo anasema kwa ujumla nyongeza ya euro 660 ni kiwango ambacho waajiri wengi hawangekifurahia. Kiwango hiki kingeweza kukubalika kama vyama vya SPD na CDU vingependekeza mabadiliko ya dhati ya malipo ya uzeeni.

Mbunge anayekaa kwa muda mrefu bungeni anaendelea kupokea msharaha unaotokana na kodi inayolipwa na raia, bila yeye mwenyewe kuwahi angalau mara moja kuigharamia mishahara ya wabunge. Na ukweli kwamba serikali ya mseto haina ujasiri wa kubadili hali hiyo, ndiyo kashfa yenyewe.