1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Josephat Charo15 Agosti 2007

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii wamezungumzia kuteuliwa kwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Abdullah Gül, na chama chake cha AK, kugombea wadhifa wa urais nchini humo, majuma matatu baada ya chama hicho kushinda uchaguzi.

https://p.dw.com/p/CHS8

Baada ya kuteuliwa rasmi, Abdalla Gül sasa anajaribu kutafuta uungwaji mkono huku kukiwa na hofu ya upinzani kwamba kiongozi huyo huenda akaibadili Uturuki kuwa taifa la kiislamu. Bwana Gül ameahidi kuilinda demokrasia na kuendelea kutenganisha taifa na dini.

Ggazeti la Frankfurter Rundschau linasema nchini Uturuki mengi yanaoneka kuwa katika hali ya wasiwasi. Nchi hiyo imefikia wakati wa mabadiliko lakini katika mkondo tofauti kuliko vile jeshi la Uturuki na Waturuki wasio na msimamo mkali wa kidini walivyofikiria katika hofu yao. Kwa maoni yake mhariri anasema kuchaguliwa kwa Abdullah Gül kuwa rais wa Uturuki hakutadunisha katiba ya nchi wala kuihatarisha demokrasia ya nchi hiyo.

Gazeti linasema ukweli ni kwamba katiba na demokrasia vitaimarika ikiwa waziri mkuu wa Uturuki, Reccep Tayyip Erdogan, wakati wa utawala wa bwana Gül, atafaulu kulionyesha jeshi mipaka yake. Kwa miaka kadhaa Umoja wa Ulaya umekuwa ukiwashawishi wanasiasa mjini Ankara wapunguze ushawishi wa jeshi katika maswala ya kisiasa na jamii. Kwa hiyo kuchaguliwa kwa bwana Gül kutakuwa hatua moja mbele kwa Uturuki kuelekea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf linasema kwa waturuki wengi inaonekana mpaka sasa kwa mtazamo wa mamwinyi wa Uturuki, yaani mapasha, hawana wasiwasi. Jeshi la Uturuki bado linabakia taasisi inayoaminiwa na Waturuki wengi. Matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge yamedhihirisha kwamba mazingira yameanza kubadilika. Asilimia 47 ya kura kwa Erdogan lilikuwa jawabu la wazi la shinikizo la mageuzi kutoka kwa maafisa.

Erdogan amefaidi kutokana na hatua ya jeshi kukataa uteuzi wa bwana Gül kuwania urais mnamo mwezi Aprili mwaka huu. Kwa mara ya kwanza katika historia Uturuki ina chama halisi kinachopendwa na raia nacho ni chama cha AK. Hata jeshi la Uturuki haliwezi kuupuza ukweli huu.

Gazeti la Nürnberger linasema swala la mtandio si dogo. Mke wa Abdullah Gül pamoja na mke wa waziri mkuu Reccep Tayyip Erdogan, wamekataa katakata kutovaa mtandio wakati wa sherehe rasmi, ambao umekuwa alama ya utambulisho wa dini ya kiislamu sio tu nchini Uturuki bali hata katika mataifa mengine.

Kwamba tabia hiyo inaweza kukubaliwa na bwana Gül na Erdogan si jambo la kushangaza, kwani hata hao wenyewe wameshawahi kufanya visa kadhaa vya kushangaza. Ukakamavu wao unaelekea mahala pamoja: Wameshawishika sana kuhusu mtandio kiasi cha kuhatarisha utawala wao na jeshi. Mahariri anasema hiyo si ishara nzuri kwa Uturuki na Ulaya.

Gazeti la Wiesbadener linamalizia kwa kusema rais wa Uturuki ana mamlaka makubwa kuliko waziri mkuu kwa hiyo ni kiongozi mkuu wa jeshi. Hofu ya jeshi la Uturuki si bure kwa kuwa chama cha AK kwa kipindi kirefu kijacho kinaweza kuzuia ushwishi mkubwa wa jeshi hilo. Na hiyo ndiyo hatua inayofaa kwa Uturuki ya sasa inayotaka kujiunga na Umoja wa Ulaya. Kwa hiyo uteuzi wa Abdullah Gül unalazimisha uamuzi wa haraka hata miongoni mwa wanajeshi.