1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

30 Julai 2007

Marekani imo njiani kukamilisha mradi wa silaha baina yake , Saudi Arabia na nchi zingine za ghuba.Shabaha ya mradi huo ni kuzuia ushawishi wa Iran katika mashariki ya kati. Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya hayo.

https://p.dw.com/p/CHSH

Katika maoni yao wahariri hao pia wanazungumzia juu ya mashindano ya mbio za baiskeli Tour de France yaliyomalizika jana.

Juu ya mradi wa silaha baina ya Marekani,Saudi Arabia na nchi zingine za ghuba, utakaogharimu dola bilioni 20 katika kipindi cha miaka 10 gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linasema kuwa lengo la mipango hiyo ya silaha ni kuzuia ushawishi wa Iran katika mashariki ya kati na kwenye eneo la ghuba. Gazeti linasema utawala wa rais Bush unaamini kwamba sasa umepata njia ya kuibana Iran.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kuwa mkakati wa kutunisha kifua , aghalabu unatumiwa na watu wanaotaka kuzima moto kwa kuumwagia mafuta.

Gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER, pia limeandika juu ya mradi huo wa silaha. Linafafanua shabaha ya mpango huo kwa kusema kuwa Marekani ina wasiwasi juu ya kile kinachoweza kutokea ikiwa itaondoa majeshi yake kutoka Irak.

Wasiwasi huo siyo hasa juu ya uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe bali juu ya ushawishi wa Iran katika mashariki ya kati na kwenye eneo la ghuba.

Lakini gazeti linasema kuwa mpango huo unathibitisha hali ya kutamauka katika utawala wa rais Bush , kwani miaka ya hivi karibuni imeonesha kuwa Saudi Arabia siyo mshiriki wa kuaminika .

Na katika maoni yake gazeti la ABENDZEITUNG kutoka mjini Munic linasema kwamba uwezo wa Marekani ,kujifunza kutokana na historia ni wa chini sana. Mhariri wa gazeti hilo anafafanua hayo kwa kuwakumbusha wasomaji wake , kwamba mnamo miaka ya nyuma Marekani ilimzaja silaha Saddam Hussein chini na juu , ili apambane na Iran. Marekani pia iliwapa silaha mataliban kuwaunga mkono katika vita vyao dhidi ya majeshi ya kisoviet yaani ya Urusi yaliyoivamia Afghanistan.

Na sasa inafanya hiyvo kwa Saudi Arabia. Mhariri anasema itaonekana hapo baadae iwapo Saudi Arabia ni mshirika wa kuaminika.Gazeti pia linakumbusha kuwa kati ya magaidi 19 walioshiriki katika mashambulio ya tarehe 11 mwezi septemba nchini Marekani 15 walitoka Saudi Arabia.

Wahariri leo pia wanazungumzia juu ya mashindano ya mbio za baiskeli Tour de France!.

Mashindano hayo yamemalizika. Na wahariri karibu wote katika maoni yao wanasisitiza jambo moja tu. Kuwa mbio hizo zenye historia ya miaka 104 , safari hii zimeacha vumbi.

Lakini vumbi hilo , anasema mhariri wa gazeti la SÜDWEST PRESSE , ni la vumba la madawa ya kuongeza nguvu, uhalifu unaoitwa doping kwa kiingereza.Hivyo basi gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linasema mapinduzi ya kuleta mwanzo mpya yanahitajika katika mashindano hayo.

AM.