1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said10 Julai 2008

Katika maoni yao leo,wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya kutekwa nyara watalii wa kijerumani nchini Uturuki.

https://p.dw.com/p/EZo1
Bendera ya chama cha PKK kinachopigania haki za wakurdi nchini Uturuki.Picha: AP

Magazeti ya Ujerumani leo yanazungumzia juu ya  kutekwa nyara watalii  wa  kijerumani nchini Uturuki.

Magazeti hayo pia  yanatoa  maoni kuhusu  mkutano wa nchi  nane tajiri uliofanyika nchini  Japan.
Kuhusu kutekwa nyara watalii wa kijerumani nchini Uturuki, wahariri wanajaribu  kuweka  mwambatano baina ya tukio hilo na harakati za  wakurdi wanaopigania haki ya  kujiamulia mambo yao  wenyewe  nchini  Uturuki.

Kwa mfano gazeti la Flensburger linasema,  chama  kinachopigania haki za wakurdi nchini  Uturuki kina  fedha za  kutosha. Ndiyo kusema  ikiwa wao ndiyo waliowateka  nyara  wajerumani hao,basi wamefanya  hivyo  kwa sababu za kisiasa na  siyo  kwa  ajili ya  fedha.


Gazeti la Dresdener Neueste Nachrichten pia  linazungumzia  kadhia hiyo kwa kutilia maanani kwamba , kwa muda  mrefu  serikali ya Uturuki imekuwa  inakanusha kuwapo tatizo  la wakurdi  nchini.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa siasa  hiyo  ilifikia  mwisho  baada ya wakurdi kupata  sehemu yao ambapo wanajiamulia mambo yao wenyewe kaskazini  mwa Irak-  yaani  jirani wa Uturuki. Kwa hiyo Kilichobakia  kwa serikali ya nchi hiyo,ni kutumia  mabavu kuwabana wakurdi  wanaowakilishwa na chama cha PKK. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha  uvamizi uliofanywa  na majeshi ya Uturuki kusini mwa Irak.

Kwa kuwa chama hicho hakiwezi kukabiliana  na serikali ya Uturuki kijeshi, kinatumia  njia  kama  hizo  za utekaji  nyara ili kuihamasisha  dunia juu ya  tatizo la wakurdi  nchini Uturiki.

Hatahivyo bado hakuna uhakika iwapo,ni PKK  iliyowateka  nyara watalii hao  wa  kijerumani.

Juu ya hayo  gazeti la Badische  Neueste Nachrichten linasema, ikiwa  itathibitika kuwa ni PKK inayowashikilia wajerumani hao ,basi tukio hilo linaashiria mwanzo wa mgogoro wa hatari.
Lakini gazeti la Neue Westfällische linahoji kuwa kitendo hicho cha utekaji nyara kinaonesha jinsi chama cha PKK kilivyotamauka.

Juu ya mkutano wa viongozi  wa nchi tajiri uliomalizika  jana  nchini Japan,

gazeti la Volkstimme  linasema  mambo yanaenda  polepole  lakini yanasonga mbele, na hasa kuhusu  suala la hali ya hewa.

Hata ikiwa India na China pia  zinabeba lawama  juu  ya kuchafuka kwa hali ya hewa, sawa  na Marekani,yafaa kutambua  kwamba  dunia  yote ni sawa na watu wanaosafiri  katika mtumbwi mmoja.

Jee  itakuwa sawa  kwa  Barack Obama kuhutubia mjini Berlin?

Mhariri  wa gazeti la  Mitteldeutsche anasema hapana. Obama  ni mjumbe wa chama  cha Demokratik aneawania urais  nchini Marekani ,kwa hiyo haitakuwa sawa kwa Ujerumani kujiingiza  katika  kampeni  yake.