1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya24 Machi 2009

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mvutano ndani ya serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/HIba
Kansela Angela Merkel na waziri wa mambo ya nje Frank Walter Steinmeier .Picha: AP

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mvutano katika serikali ya mseto ya Ujerumani, na juu ya mpango mwingine wa kufufua uchumi nchini Marekani.

Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya hali ya watoto nchini Ujerumani.

Juu ya mvutano uliopo ndani ya serikali ya mseto ya Ujerumani wakati, imebakia miezi sita tu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu hapa nchini gazeti la Fuldauer linasema kauli zinazosikika kutoka kwa wawakilishi wa serikali hiyo zinathibitisha ugumu wa ndoa ya kufinyanza!

Mhariri wa gazeti hilo anasema mvutano huo unathibitisha kwamba kisichokuwa na nasaba ya pamoja hakiwezi kuenda pamoja.Gazeti linasema mvutano huo umefikia kiwango cha kutisha kwa sababu, unahatarisha hata msimamo wa pamoja juu ya kudumisha nafasi za ajira katika kiwanda cha magari kama cha Opel.


Mhariri wa gazeti la Darmstäter Echo pia anazungumzia juu ya serikali ya mseto kwa kutilia maanani kwamba imebakia miezi michache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.Mhariri huyo anatilia maanani mtazamo wa vyama vikuu vilivyomo katika mseto huo,SPD na CDU wa kuhakikisha kwamba vitaendelea kuongoza hadi hapo uchaguzi utakapofanyika.

Wahariri wa magazeti ya Main Echo na Berliner Morgenpost wanazungumzia juu ya mustakabal wa watoto nchini Ujerumani.Mhariri wa Main Echo anasisitiza kuwa watoto ni hazina kubwa ya siku za usoni.Kutokana na hayo anasema pana haja ya kuwekeza fedha, kwa ajili ya shule za matayarisho,sehemu za malezi na sehemu nyingine ambapo watoto wanaweza kupatiwa chakula kizuri.Anasema hatua hizo zitakuwa sawa na vitega uchumi kwa manufaa ya siku za usoni.

Na mhariri wa Berliner Morgenpost anasema badala ya kuwapa watoto fedha zaidi, wanahitaji kupewa malezi bora na kutambua kwamba uwezo wao unathaminiwa.

Gazeti la Kieler Nachrichten linatoa maoni juu ya mpango mwingine wa Marekani wa kuyaokoa mabenki.Mhariri wa gazeti hilo anasema mpango huo ni ishara dhahiri ya kutapatapa.Gazeti linasema ingawa Marekani imeshamimina lukuki za fedha katika mabenki, bado haijatatua kiini kilichosababisha mgogoro mkubwa wa uchumi.



Mwandishi:Abdul Mtullya/ Zeitungen

Mhariri:Abdul-Rahman