1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
27 Desemba 2017

Wahariri wameandika juu ya ujumbe wa Krismasi wa rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kwa Wajerumani na pia uamuzi wa tume ya uchaguzi ya nchini Urusi wa kumzuia mpinzani Navalny kushiriki katika uchaguzi wa urais.

https://p.dw.com/p/2pz5C
Weihnachten mit dem Bundespraesidenten
Picha: picture-alliance/SvenSimon

Volksstimme

Mhariri wa gazeti la Volksstimme anasema katika hotuba yake ya kwanza ya Krismasi kama rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amewasilisha ujumbe uliokuwa wazi kabisa. Steinmeier ametahadharisha kwamba hali ya utulivu  iliyopo nchini inaweza kugeuka na kuwa ya hatari. Mhariri huyo wa gazeti la Volksstimme anasema uhaba wa madaktari, kufungwa shule na kupungua huduma muhimu za benki katika sehemu za vijijini ni mazingira yanayoweza  kufanya hali ilipuke. Ndiyo sababu ujumbe wa rais wa Ujerumani kwa viongozi na wananchi ni muhimu anasema mhariri wa gazeti hilo.

Süddeutsche Zeitung

Lakini mhariri wa Süddeutsche Zeitung hakuridhika na ujumbe wa rais Steinmeier, anasema haitoshi kutoa wito juu ya kuwa na subira tu. Mhariri huyo anafafanua kwamba mtu angelifurahi kusikia maneno ya kuonyesha kwamba rais wa Ujerumani amesimama safu moja na wananchi kwamba anaonana na wananchi ana kwa ana. Katika hotuba yake bwana Steinmeier angelieleza wazi kwamba juhudi binafsi za wananchi haziwezi kuchukua nafasi ya wajibu wa serikali. Mhariri wa Süddeutsche anasisitiza katika maoni yake kwamba serikali lazima itimize wajibu wake kwa kuhakisha kwamba miundombinu ya kijamii inadumishwa. 

Tagesspiegel

Nalo gazeti la Tagesspiegel linasema katika hotuba yake, rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier angelipaswa kuzama zaidi katika hali halisi inayoikabili nchi. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba mtu anajiuliza iwapo kweli anaishi kwenye nchi ya asali na maziwa, wakati katika upande mwingine wapo watoto zaidi ya milioni moja na nusu wenye wazazi wanaopokea misaada ya serikali pia wapo wastaafu wapatao laki tatu na nusu wanaotegemea kupewa chakula cha hisani mara kwa mara.

Mhariri wa tagesspiegel anasema watu wengi watakuwamo katika hatari ya kukumbwa na umasikini katika siku zijazo nchini Ujerumani. Watu wengi sasa hawawezi kukidhi kwa ukamilifu mahitaji ya familia zao licha  ya kuwa na ajira, pamoja na hayo kodi za nyumba hazishikiki. Mhariri huyo  wa gazeti la Tagesspiegel anasema Ujerumani sasa imegawika sehemu mbili katika huduma za afya.

Frankfurter Rundschau

Vilevile wahariri wa magazeti wametoa maoni juu ya uamuzi wa tume ya uchaguzi ya nchini Urusi wa kumzuia kushiriki kwenye uchaguzi wa rais kiongozi wa upinzani nchini humo Alex Navalny ambapo alitaka kushindana na rais Vladimir Putin katika uchaguzi wa urais wa mwezi Machi mwakani. Mhariri wa Frankfurter Rundschau anasema sababu ya tume ya uchaguzi ya kumkataza Alex Navalny kugombea ni kwamba amekuwa mshindani mkali wa Vladimir Putin lakini mhariri pia anautilia maanani mkakati wa kiongozi huyo wa upinzani juu ya mwito wake wa kususia uchaguzi. Mhariri huyo anauliza iwapo mkakati huo utakuwa na maana yoyote?. 

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:  Gakuba, Daniel