1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya2 Julai 2009

Wahariri wa magazeti ya hapa nchini wasema, pana haja ya kufafanua dhima ya jeshi la Ujerumani.

https://p.dw.com/p/IfZG
Askari wa Ujerumani nchini Afghanistan.Picha: picture-alliance/ dpa


Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya siku ya wakulima wa hapa nchini, juu ya jukumu la wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanstan na matukio ya nchini Iran.


Gazeti la Flensburger Tageblatt linalozungumzia juu ya siku ya wakulima hapa nchini linawalaumu wakulima kwa kujipalia makaa wao wenyewe.


Gazeti hilo linasema wakulima wa Ujerumani wana haki ya kudai kurejeshwa kwa ushindani wa haki lakini kuhusu bei ya maziwa wakulima hao kwa kiasi kikubwa wamejipalia makaa. Mhariri wa gazeti la Flensburger Tageblatt anaeleza kuwa katika nyakati ambapo bei za mazao ni nzuri siyo sahihi kuzalisha mazao mengi. Gazeti linasema anaefanya hivyo asishangae kuona masoko mapya yakianzishwa na yeye akiwa nje ya masoko hayo.

Na gazeti la Allgemeine Zeitung pia linazungumzia juu ya ushindani katika soko la mazao ya kilimo nchini Ujerumani, kwa kuwakumbusha wakulima kwamba sasa dunia imo katika mchakato wa sera za utandawazi.

Gazeti hilo linafafanua kwa kusema,kwamba gurudumu la sera za dunia utandawazi halitarudi nyuma tena.

Umoja wa Ulaya hautaweza kuendelea kutoa ruzuku kuwafidia wakulima wa Ulaya ili waweze kushindana kwenye soko la dunia.

Mhariri wa gazeti la Allgemeine Zeitung anawashauri wakulima wa Ujerumani, juu ya kutafuta mkakati utakaowawezesha kuenda sambamba na nyakati za sasa.


Uchunguzi uliofanyika hivi karibuni umeonesha kwamba asilimia 61 ya wananchi wa Ujerumani wanataka majeshi ya nchi yao yaondoke Aghanistan. Juu ya hayo mhariri wa gazeti la Südwest Presse anasema kuwa wanajeshi wa Ujerumani sasa wanakabiliwa na hali halisi nchini Afghanistan ingawa serikali inajaribu kutoa picha kwa lengo la kuonesha kwamba wanajeshi hao wanafanya kazi za msamaria mwema nchini Afghanistan. Gazeti hilo linaeleza kwamba serikali ya Ujerumani inawataka wananchi wake waamini kwamba jeshi lao linatoa misaada ya kibinadamu katika kutekeleza majukumu ya kimataifa. Hatahivyo gazeti hilo linasema wakati umefika wa kufanyika mjadala juu ya dhima mpya ya jeshi la Ujerumani.

Utawala wa Iran unahitaji kuwa na adui wa nje ili kuweza kudhibiti hali ya ndani. Gazeti la Braunschweiger linatoa maoni hayo.Gazeti hilo linasema, kana kwamba wanatumia kitabu cha masomo ya propaganda, viongozi wa Iran wanazilaumu nchi za magharibi kwa kuchochea mgogoro ndani ya nchi yao.

Viongozi hao wanatafuta adui wa nje ili kuwahadaa wananchi wao juu ya hali ya ndani. Lakini, gazeti linsema , bila shaka viongozi hao wameshangazwa kuona jinsi vijana wao wanavyopenda umarekani.

Mwandishi/Mtullya/dt zeitungen

Mhariri/Abdul-Rahman