1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya4 Machi 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya hatua zilizochukuliwa na Ugiriki ili kuyakabili matatizo yake ya bajeti.

https://p.dw.com/p/MJsf
Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya Ugiriki katika juhudi za kuepuka kufilisika.

Serikali ya Ugiriki imetangaza mpango wa kubana matumizi utakaookoa kiasi cha Euro bilioni 4.8. Pamoja na hatua hizo ni kuongeza kodi ya mauzo kwa asilimia 2, kuongeza kodi ya tumbaku na ya mafuta. Na wastaafu hawataongezewa pensheni.

Hatua hizo na nyingine zimechukuliwa ili kuiepusha nchi hiyo kufilisika.

Juu ya hatua hizo, mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung anasema sambamba na kutekeleza kwa moyo wote hatua ilizopitisha,Ugiriki sasa inahitaji kuungwa mkono na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Mhariri huyo anaeleza kuwa kwa wiki kadhaa Ugiriki ilikuwa inabanwa na walanguzi waliojaribu kuifilisi nchi hiyo. Na ndiyo sababu anasema mharriri huyo,ni muhimu kwamba Umoja wa Ulaya sasa unatafakari hatua za kuyadhibiti masoko ya mitaji.

Mhariri wa gazeti la Financial Times Deutschland anasema serikali ya Ugiriki imepiga hatua ndefu sana katika uamuzi wake,lakini siyo katika wakati mwafaka. Gazeti hilo linafafanua kwa kusema hatua kali aghalabu hazisaidii ikiwa zinapitishwa katika wakati usiofaa. Pamoja na hayo,maamuzi hayo yanaweza kuzuia vitega uchumi na kuwalazimisha wananchi wabanie fedha zao mifukoni. Gazeti la Financial Times Deutchland linasema tume ya Umoja wa Ulaya inapaswa kuyatilia hayo maanani itakapotathmini hatua zilizotangazwa na Ugiriki. Gazeti hilo linasema nchi hiyo inahitaji mageuzi yatakayoleta manufaa mnamo kipindi kifupi.

Hatua zilizotangazwa na serikali ya ugiriki ni kali ikiwa pamoja na kupunguza malipo ya uzeeni na kupandisha umri wa kustaafu. Lakini Wagiriki siyo watu pekee wanaokabiliwa na hatua kama hizo hayo anayasema mhariri wa gazeti la Flensburger Tageblatt.

Mhariri huyo anaeleza kuwa nchini Ujerumani vilevile fedha za krismasi na malipo ya wastaafu zilipunguzwa. Anasema nchini Ujerumani vilevile kodi ya mauzo imepandishwa. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kuwahurumia Wagiriki,kwani ni serikali yao iliyokuwa inaishi nje ya uwezo wake kwa muda wa miaka mingi. Hata hivyo, inapasa kuzitambua juhudi zilizochukuliwa na serikali ya nchi hiyo ili kuleta mabadiliko.

Na mhariri wa gazeti la General Anzeiger anatahadharisha kwamba, ikiwa Ugiriki haitafanikiwa katika juhudi za kukabiliana na mgogoro wake wa bajeti, sarafu ya Euro inaweza kuwa mashakani.!

Mhariri wa General Anzeiger anasema hayo kwa kutilia maanani kwamba pana nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zinazokabiliwa na matatizo ya bajeti vilevile, kama Uhispania na Ureno.

Mwandishi/ Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Miraji Othman