1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya12 Oktoba 2010

Wahariri wa magazeti leo pia wanazungumzia juu ya matamshi ya waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer juu ya wahamiaji.

https://p.dw.com/p/PcTT
Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer aliesimama nyuma ya Kansela Angela Merkel.Picha: picture alliance/dpa

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo pia wanazungumzia juu ya matamshi yaliyotolewa na waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer. Waziri Mkuu huyo alisema kuwa Ujerumani sasa haina nafasi tena kwa wahamiaji kutoka tamaduni za kigeni.
Juu ya hayo gazeti la Donaukurier linatilia maanani kwamba Seehofer sasa anarudi nyuma .Waziri mkuu huyo amesema kuwa alieleweka vibaya.

Hata hivyo mhariri wa Donaukurier anasema kwa kutoa kauli hiyo Seehofer alitaka kuonekana kuwa mwanasiasa anaetoboa ukweli.

Mhariri wa gazeti la Berliner Morgenpost pia anazingatia mjadala uliozuka nchini Ujerumani hivi karibuni juu ya Uislamu.Anasema kuwa wapo mamilioni ya waislamu ambao ni sehemu ya Ujerumani. Na hivyo basi kujaribu kusema kwamba Ujerumani inavamiwa na utamaduni wa kigeni, kama waziri Mkuu Seehofer alivyosema, ni jambo la upuuzi.
Lakini gazeti la Frankfurter Rundschau linatilia maanani kuwa mjadala uliozuka nchini Ujerumani juu ya Uislamu unaonyesha kuwa viongozi wa Ujerumani wamegawanyika katika pande mbili.

Gazeti hilo linaeleza kuwa katika upande mmoja ni wale kama rais wa Ujerumani Christian Wulff wanaotambua kwamba Ujerumani ni jamii iliyo wazi, na katika upande mwingine ni wale wanaojaribu kutia zege ili kuziba kila kitu.

Katika maoni yake leo mhariri wa gazeti la Flensburger Tageblatt anasisitiza kwamba Ujerumani ni nchi inayohamiwa na watu kutoka duniani kote.Na hiyo ni hali halisi.Kinachohitajika sasa ni mjadala wa dhati juu ya suala hilo.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linazungumzia juu ya hali ya kisiasa nchini Kirgistan na linasema kuwa wale wanaouunga mkono utawala wa hapo awali bado wana nguvu.Gazeti hilo linaeleza kuwa wale wanaomwuunga mkono Rais wa hapo awali, Bakiyev aliengushwa hivi karibuni bado wana nguvu.Watu hao watatumia kila ombwe, yaani kila pengo lililopo kwa manufaa yao. Kwa hiyo serikali mpya inapaswa kuwapa watu wa Kirgistan uhakika kwamba mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni yataleta manufaa kwao.

Wajerumani wawili wamekamatwa nchini Iran kwa kosa la kuingia nchini humo kama watalii lakini kumbe ni waandishi habari waliokuwa wanataka kufanya uchunguzi wa mkasa wa Ashtiani, mwanamke aliehukumiwa adhabu ya kifo kwa kupigwa mawe.Juu ya waandishi hao,gazeti la Badische linasema:waandishi hao wamejitosa katika hatari kubwa sana, na siyo kwao binafsi.

Gazeti la Badische Zeitung linatilia maanani kwamba jambo la kuhofia sasa ni kwamba wakili mama huyo Sakine Ashtiani pia atakuwa hatarini.Pia pana hatari ya Iran kuwatumia waandishi hao kama mateka.

Mwandishi/ Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen...

Mhariri/ Josephat Charo.