1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti.

16 Julai 2007

Katika maoni yao, wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya uamuzi wa Urusi kujiondoa kwenye mkataba wa kudhibiti silaha za kawaida barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHSP


Pia wanazungumzia juu ya msimamo wa rais wa Ujerumani Horst Köhler kuhusu mapendekezo yaliyotolewa hivi karibuni na waziri wa mambo ya ndani bwana Wolfgang Schäuble.

Juu ya uamuzi wa Urusi kujitoa kwenye mkataba wa kudhibiti silaha za kawaida barani Ulaya mhariri wa gazeti la FRANKURTER ALLGEMEINE anasema kuwa Urusi imepitisha uamuzi huo kutekeleza msimamo wake uliotangazwa mwezi wa aprili, kama jibu la mpango wa Marekani juu ya kuweka ulinzi dhidi ya makombora katika nchi za Ulaya mashariki.

Urusi sasa imeamua kujitoa kwenye mkataba huo ili iweze kuyahamisha majeshi yake namna ipendavyo katika eneo lake.

Lakini mhariri anasema Urusi tayari imekuwa inafanya hivyo siku nyingi katika Chechnya kwa lengo la kupambana na magaigi ,kama inavyosema.

Mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG anasema kuwa uamuzi wa Urusi siyo jambo la kushangaza.

Anaeleza kuwa tokea hapo awali Urusi kwa kiwango kikubwa imekuwa inasimama kando ya mkataba huo.

Lakini gazeti linaeleza ,kuwa kutokana na hatua hiyo, uhusiano baina ya Urusi na nchi za magharibi hautakuwa rahisi.

Wahariri leo pia wanazungumzia juu ya ushauri wa rais wa Ujerumani Horst Köhler kwa waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble.

Rais Köhler ametoa lawama kali dhidi ya waziri Schäuble kutokana na kauli za waziri huyo za hivi karibuni kuhusu mipango yake ya kupambana na ugaidi.

Schäuble alisema hivi karibuni, kuwa ikibidi haitakuwa vibaya kuua , katika kupambana na magaidi.

Juu ya hayo rais Köhler amemshauri waziri Schäuble awe mwangalifu anapotoa kauli kama hizo.

Juu ya hayo gazeti la NEUE PRESSE linasema rais Köhler ametoa ushauri kwa waziri huyo baada ya kubaini kwamba mambo yanaweza kuenda mrama. Mhariri wa gazeti hilo anasema ,rais Köhler ametoa ishara kuwa shughuli haziwezi kuendelea kana kwamba hakuna kilichotokea , yaani mapendekezo ya kiherehere yaliyotolewa na waziri wa mambo ya ndani, ikiwa pamoja na juu ya kuua ikiwa itabidi, katika kupambana na watuhumiwa wa kigaidi.

AM.