1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

23 Aprili 2007

Miaka 30 baada ya kundi la kigaidi kumwuua aliekua mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani Siegfried Buback mkasa huo bado unaendelea kufuatiliwa hadi leo. Katika maoni yao wahariri wa magazeti leo wanazingatia suala hilo.

https://p.dw.com/p/CHTA

Mhariri wa gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND anasema kuwa sehemu ya historia ya Ujerumani inadhihirika mbele ya macho ya kila mtu kutokana na habari mpya kusikika juu ya kuuawa kwa mwendesha mashtaka Sigfried Buback mnamo mwaka 1977 na kundi la kigaidi la Red Army.Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba aliehukumiwa adhabu ya kifungo Christian Klar siye aliemwuua mwendesha mashtaka huyo.

Gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE kutoka Bielefeld linaangalia kwa umaizi uhalifu uliotoendwa na kundi hilo la kigaidi na linasema katika maoni yake kuwa, licha ya hukumu zilizotolewa dhidi ya wauaji wa kundi hilo, siyo sawa kusema kwamba uchunguzi juu ya uhalifu wa kundi hilo umefanyika kwa mafanikio kabisa. Kati ya mauaji 22 yaliyofanywa na magaidi wa kundi hilo ni mawili tu yaliyoweza kuchunguzwa kwa mafanikio.


Mhariri wa gazeti la DIE WELT anasema katika maoni yake kwamba enzi ya kundi la Red Army bado haijatamatika kabisa la sivyo vipi inawezekena hadi leo kuwapo watu wanaotoa habari juu ya mkasa uliotokea miaka 30 iliyopita. ?


Gazeti la kila wiki der Spiegel linadai kwamba lina ushahidi kwamba ni mtu mwengine aliemwuua mwanasheria Sigfried Buback.

Mhariri wa gazeti la die RHEIN kutoka mji wa Koblenz amezungumzia juu ya hayo katika maoni yake kwa kusema , ikiwa madai ya gazeti la der Spiegel ni ya kweli basi, idara kuu ya kupambana na uhalifu pamoja na idara ya ulinzi wa katiba zilikuwa na habari juu ya ukweli wa mkasa huo tokea miaka 20 iliyopita. Hivyo basi idara za sheria ziliwekwa katika kiza na uzuzu kwa muda wote huo. Mhariri anasema hiyo ni kashfa ya hali ya juu.

.Lakini mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG anasema , kutokana na kazi iliyofanywa na idara za sheria, yumkini, sasa wajerumani wanakaribia kufichua kashfa kubwa sana katika sekta ya sheria.

Mhariri huyo anasema ikiwa mhalifu wa kweli amekua anafaidi uhuru kwa miaka yote hiyo 30 , na mtu asiyekuwa na hatia ndiye alieadhibiwa kwa sababu tu idara zinazohusika hazikupeleka ushahidi mahala panapostahili, japo zilijua fika kilichojiri , basi taasisi nzima ya mahakama hapa Ujerumani itatikisika zaidi kutokana na kashfa , kuliko na mabomu ya kundi la Red Army.

Na gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linasema kuwa yumkini kundi la kigaidi la RAF limevunjwa, lakini anatahadharisha kuwa , baadhi ya wanachama wa kundi hilo bado wanaendelea kuwa na fikara za hapo awali . Gazeti linasema ukimya wa Christian Klar, aliehukumiwa kifungo japo yeye siye mwuuaji unamaanisha kuwa huenda ikawa anaficha ushahidi mwingine.