1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa masoko ya fedha.

Mtullya, Abdu Said18 Machi 2008

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya hatua zilizochukuliwa na benki ya Marekani kuukabili mgogoro wa fedha duniani.

https://p.dw.com/p/DQZf
Pilikapilika kwenye soko la hisa nchini Ujerumani-DAXPicha: AP



Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mgogoro unaoyakabili masoko ya fedha duniani.

Licha ya hatua iliyochukuliwa na Benki Kuu ya Marekani kuteremsha kiwango cha riba na licha ya hatua ya benki ya JP Morgan Chase kuichukua benki ya vitega uchumi, Bear Sterns mgogoro kwenye masoko ya fedha duniai umeendelea kushtadi.

Juu ya hatua hizo mhariri wa gazeti la FRANKFUTER ALLGEMEINE anasema mkakati wa kupunguza viwango vya riba ili kuukabili mgogoro huo siyo sahihi- na ndio kwanza unachangia katika kuvuruga wajihi wa benki kuu ya Marekani- yaani hazina kuu ya fedha duniani.

Gazeti hilo linaeleza kuwa hali haijawa nzuri wakati ambapo mfumuko wa bei unaongezeka.

Na jinsi mgogoro huo utakavyoendelea hakuna anaeweza kutabiri, lakini pana uwezekano mkubwa wa hali kuwa mbaya zaidi, anasema mhariri wa gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE.


Gazeti la NORDBAYERISCHE KURIER kutoka jimbo la Bavaria pia linazungumzia juu ya mgogoro huo kwa kusema watu wamepoteza imani juu ya uwezo wa taasisi za fedha za kimataifa.

Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema, hatua zilizochukuliwa na benki kuu ya Marekani asilani hazitarejesha imani ya watu -ni kinyume cha hayo, hatua hizo zinathitibisha ukubwa wa mgogoro uliopo.

Mgogoro wa fedha duniani pia umeonesha hulka halisi ya taasisi za fedha- hakuna anaetaka kumsaidia mwengine kwa nia ya dhati.

Hayo anaeleza mhariri wa gazeti la DER SCHWARZWÄLDER BOTE.

Anasema msukosuko wa fedha uliopo sasa unaonesha ni kitu gani kinaweza kutokea ikiwa mashirika makubwa ya fedha yanaendekeza uroho wa fedha.

Imani juu ya benki za watu binafsi imeingia ufa na hayo yanasababisha wasiwasi katika uchumi wa dunia.

Kutokana na hayo gazeti linashauri kuazishwa utaratibu wa kudhibiti shughuli za benki hizo duniani kote.

Na gazeti la MANNHEIMER MORGEN linasisitiza hayo kwa kusema, sumu ya biashara ya fedha na masoko ya hisa ni hali ya wasi wasi na kutokuwapo imani.

Tatizo la madeni limeyakumbuka masoko ya fedha na hatua zinazochukuliwa sasa na mameneja zinaongeza tu wasiwasi uliopo. Imani imeshapotea, kiasi kwamba hata hatua ya kuteremsha kiwango cha riba haitasaidia tena kuyanasua mabenki yaliyonasa katika mtego wa madeni.