1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wazungumzia juu mabadiliko ya hali ya hewa.

Abdu Said Mtullya9 Desemba 2009

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo pia wanazungumzia juu ya mkutano wa mjini Copenhagen.

https://p.dw.com/p/KyKo
Wanaharakati wa ulinzi wa mazingira wakiandamana kusisitiza umuhimu wa kufikia mapatano mjini Copenhagen.Picha: AP

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya mkutano unaojadili tishio la mabadiliko ya hali ya hewa, mashambulio ya kigaidi nchini Irak na juu ya adhabu ya faini iliyotolewa kwa chama cha kiliberali- FDP.

Juu ya mkutano unaojadili tishio linalotokana na mabadiliko ya hali ya hewa gazeti la Nordwest-Zeitung linasema pana hatari kubwa ya mkutano huo kumalizika kwa mafanikio finyu kutokana na mtazamo wa kuweka mbele maslahi ya kitaifa yanayozuia njia ya kufikia mapatano ya kimataifa.

Hatahivyo gazeti la Nordwest Zeitung linasema bado pana ishara ya matumaini ,hasa kutokana na uamuzi wa rais Obama kusema kwamba atashiriki katika vikao vya mwisho vya mkutano wa mjini Copenhagen.

Gazeti hilo linasema kushiriki kwa Obama kwenye mkutano huo kutajenga imani. Hatahivyo mhariri wa Nordwest-Zeitung anaeleza kwamba kipimo cha imani hiyo kitaonekana katika kauli atakazozitoa.

Gazeti la Münchner Merkur linatathmini upande wa biashara wa suala la mabadiliko ya hali ya hewa.

Linasema kuhusu ulinzi wa mazingira,wajasiramali hawalengi shabaha ya kutenda wema bali, wanazingatia maslahi ya kibiashara. Kwa sababu bidhaa wanazozitengeneza , za kupunguza utoaji wa gesi chafu, aghalabu zinapunguza matumizi ya mafuta na gesi. Kwa hiyo ,anasema mhariri wa gazeti la Münchner Merkur, kwamba soko ndilo linaloamua juu ya nani anafanya biashara ya bidhaa za ulinzi wa mazingira, na siyo mkutano wa mjini Copenhagen.


Chama cha kiliberali FDP kilichomo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani kimepewa adhabu ya kulipa faini ya Euro milioni 4 na laki tatu kwa kosa la kupokea michango kinyume na sheria. Aliepokea michango hiyo alikuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, hayati Jürgen Möllemann. Juu ya hayo gazeti la Mannheimer Morgen linasema kupokea fedha hizo lilikuwa jambo baya,lakini jambo baya zaidi ni kwamba fedha hizo zilitumiwa kwa ajili ya kuchapisha vipeperushi vya chuki dhidi ya wayahudi.

Kwa hiyo kulipa faini,hiyo ni fursa kwa chama cha FDP ya kufunga ukarasa wa kisirani katika historia yake.

Na Gazeti la Braunschweiger Zeitung linazungumzia juu ya mashambulio ya kigaidi nchini Irak kwa kusema kwamba njia ya pekee ya kukomesha mashambulio hayo ni kwa majeshi ya kigeni kuondoka nchini humo.

Mwandshi Mtullya Abdu/ Deutsche Zeitungen

Mhariri/Abdul-Rahman