1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani juu ya Mashariki ya kati.

Abdu Said Mtullya28 Septemba 2010

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni yao juu ya uamuzi wa Israel kutorefusha muda wa kusimamisha ujenzi wa makaazi ya walowezi.

https://p.dw.com/p/PP8f
Rais wa Mamlaka ya ndani ya wapalestina Mahmoud Abbas.Picha: AP

Mazungumzo juu ya kuutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati yamo katika hatari ya kuvunjika kutokana na msimamo wa Israel wa kuanza tena ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya suala hilo.

Mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche Zeitung anazungumzia juu ya zege la kisiasa katika upande wa Israel linalozuia njia ya kuekelekea kwenye suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Mhariri wa gazeti hilo anasema kuwa serikali ya Israel inatambua hayo vizuri sana.Mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche Zeitung anasema Israel inapanga mawe ili kuziba njia ya kufikia suluhisho.Gazeti hilo linatahadharisha kwamba hatua ya Israel ya kuanza tena kujenga makaazi ya walowezi wa kiyahudi inayapa makundi yenye siasa kali sababu ya kuyakindua mazungumzo yanayofanyika sasa juu ya kuleta suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Mhariri wa gazeti la Hamburger Abendblatt pia anasema mazungumzo juu ya kuleta amani katika Mashariki ya Kati yamo hatarini kuvunjika, na anaeleza kuwa walowezi wa kiyahudi sasa wanaruhusiwa kujenga makaazi 2000 mapya katika Ukingo wa Magharibi bila ya kuomba kibali.

Makaazi hayo alfu mbili maana yake ni viunzi 2000 vinavyozuia njia ya kuelekea kwenye suluhisho.

Baada ya muda wa wiki nne tu tokea yaanze, mazungumzo hayo, sasa yamo hatarini kuvunjika, kabla hata wajumbe hawajavifikia visiki, kama masuala ya mipaka, wakimbizi wa kipalestina na mji wa Jerusalem.
Lakini pamoja hayo yote mhariri wa gazeti la Hamburger Abendblatt anasema bado ni hatua ya mafanikio kwamba rais wa Mamlaka ya ndani ya wapalestina Mahmoud Abbas hajasimama na kutoka nje.

Lakini mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine anatilia maanani kwamba Mahmoud Abbas anasubiri uamuzi wa Umoja wa nchi za kiarabu juu ya hatua ya kuchukua.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kuwa Mahmoud Abbas anasubiri uamuzi wa nchi nyingine za kiarabu iwapo andelee na mazungumzo ama ayaachilie mbali. Na anausubiri uamuzi huo wakati ambapo mazungumzo mengine yanafanyika mjini Damaskus juu ya kuwapatanisha Hamas na wapalestina wengine wote

Gazeti la Frankfurter Neue Presse linasema Mahmoud Abbas amekwama kwa sababu Israel haipo tayari kurudi nyuma.

Mwandishi Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman