1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti,Ujerumani

13 Machi 2007

Rais Jacques Chirac wa Ufaransa ameamua kung’atuka baada ya kuitumikia nchi yake kwa miaka zaidi ya 40. Jee nani atamrithi, na atakabiliwa na changamoto zipi? Hilo ndilo suala linalozingatiwa na wahariri wa magazeti katika maoni yao leo.

https://p.dw.com/p/CHTW

Akizungumzia juu uamuzi mwanasiasa huyo mashuhuri, mhariri wa gazeti la BERLINER ZEITUNG anasema kuwa yeyote yule atakaemrithi bwana Chirac , atapaswa kuwa na ujasiri wa kupiga kifua na kusema wazi aliyonayo moyoni sambamba na kuwa na ujasiri wa kupeleka kata mtungini.

Mhariri wa gazeti hilo anasema ,iwe ni Sarkozy ama bibi Royal waliomo katika kinyang’anyiro cha kugombea kiti cha urais, yeyote kati ya hao, au hata mwingine, atapaswa kuchukua hatua za kupunguza deni kubwa la nchi ;- takwimu zinaonesha kuwa kila mtoto anazaliwa na deni la Euro alfu 18 nchini Ufaransa.

Mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ODERZEITUNG anatilia maanani kwamba bwana Chirac anaondoka bila ya kumpendekeza mtu yeyote wa kumrithi.

Naye mhariri wa gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT anapiga urari wa kazi aliyofanya rais Chirac.

Kuhusu ndani ya nchi, mhariri huyo anasema, aliyotimiza bwana Chirac ni uchinjo, yaani kidogo…ustawi wa uchumi ni dhaifu, watu wengi hawana ajira na deni la nchi ni kubwa.

Mhariri anatamka kuwa bwana Chirac anawaachia wafaransa kazi ngumu.

Mhariri wa gazeti la FRÄNKISCHE TAG anakubaliana na tathmini hiyo kwa kueleza kuwa bwana Chirac hakuweza kujenga urari wa kijamii nchini. Matokeo yake yalikuwa ghasia zilizovikumba vitongoji kadhaa mjini Paris mnamo mwaka 2005.

Gazeti linasema kuwa wafaransa wameshapewa ahadi nyingi sana, lakini sasa kinachohitajika ni matendo, yumkini kutoka kwa mwana mama , kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Ufaransa, yaani bibi Royal mgombea wa chama cha kisoshalisti, ikiwa atashinda katika uchaguzi.

Na Abdu Mtullya.