1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI.

Abdu Said Mtullya4 Januari 2011

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya kushambuliwa Wakristo nchini Misri.

https://p.dw.com/p/ztLV
Wakristo wanashambuliwa nchini Msiri.Picha: dapd

Wahariri wa magazeti karibu yote leo wanazungumzia juu ya mashambulio yaliyofanywa na wana itikadi kali wa kiislamu katika kanisa la mjini Alexandria, nchini Misri.Wahariri hao wanazitaka serikali za nchi za magharibi zichukue hatua madhubuti ili kuwalinda Wakristo katika nchi za kiarabu.Na hivyo ndivyo anavyosisitiza mhariri wa gazeti la Lausitzer Rundschau katika maoni yake.

Mhariri huyo anasema sasa wakati umefika kwa nchi za magharibi kuzikazia macho zile zinazoitwa serikali za kirafiki katika Mashariki ya Kati.

Gazeti la Trierischer Volksfreund linasema hii siyo mara ya kwanza kwa Wakristo kuuawa katika nchi za kiarabu. Kwa hiyo huu sasa siyo wakati wa kuziendekeza itifaki za kidiplomasia.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa wamarekani, wayahudi, wawakilishi wa mashirika ya misaada na watalii wameshambuliwa katika nchi za kiarabu mara kwa mara. Na sasa vitisho vya wanaitikadi kali dhidi ya Wakristo wa madhehebu ya Coptic vimefika hadi Ujerumani.Katika hali hiyo, matamko ya kidiplomasia sasa hayafai. Lazima serikali za nchi za magharibi zichukue hatua thabiti.

Katika maoni yake, mhariri wa gazeti la Reutlinger Generalanzeiger anasema kuwa mwito uliotolewa na Rais Hosni Mubarak kuwataka Wakristo na Waislamu wasimame pamoja dhidi ya magaidi ni unafiki. Sababu ni kwamba Uislamu ndiyo dini rasmi nchini Misri.

Ikiwa Rais Mubarak ana dhamira ya kweli, basi atapaswa kuyabadili mambo mengi sana nchini mwake. Misri imo katika hali nyeti na Rais Mubarak hawezi kuendelea kuyapuuza malalamiko yanayotolewa duniani kote.Mambo yanaweza kwenda mrama zaidi nchini Misri kiasi cha nchi hiyo kuweza kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe .

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anatalia maanani kwamba kwa wanaitikadi kali wa Kiislamu,mashambulio dhidi ya Wakristo katika nchi za Mashariki ya Kati ni kisasi kwa vita zinazoendeshwa na serikali za nchi za magharibi. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kuwa wanaitikadi kali wa Kiislamu, serikali za magharibi zinazoendesha vita ni za Kikristo. Kwa hiyo kinachoitwa mapambano ya kitamaduni siyo jambo la nadharia kwa wanaitikadi kali hao katika nchi za Kiarabu.Kwa hiyo shambulio lolote ni shambulio la kisasi.

Lakini katika maoni yake, gazeti la Berliner Zeitung linakumbusha kwamba Waislamu pia wanauawa kutokana na mashambulio ya kigaidi na linaeleza kuwa mashambulio yaliyofanywa kanisani katika mji wa Alexandria yana lengo la kuishinikiza serikali ya Misri. Lakini mashambulio ya kigaidi yamesababisha vifo vya Waislamu vile vile. Kwa hiyo,kwa nchi za magharibi kujaribu kuonyesha kwamba Wakristo ndiyo wanaonewa, ni propaganda tupu.

Mwandishi:Mtullya Abdu

Mhariri: Miraji Othman