1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI.

Abdu Said Mtullya10 Novemba 2011

Wahariri wa magazeti watoa maoni juu ya Iran na mgogoro wa madeni.

https://p.dw.com/p/138Ed
Roketi za Iran.Picha: IRNA

Wahariri wamagazeti leo wanauzungumzia mpango wa nyuklia wa Iran na mgogoro wa madeni unaozikabili nchi za Ulaya.

Juu ya Iran gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema kuwa nchi hiyo inataka kuwa na silaha za nyuklia na huenda ikaziunda silaha hizo. Kwa hivyo kwa nini jumuiya ya kimataifa haiwezi kuiambia Iran wazi kwamba kuna kitu kinachoitwa shambulio la kisasi ikiwa itazitumia silaha hizo?

Mhariri wa Frankfurter Allgemeine anasema hiyo ni njia ya kutisha,lakini ili kuizuia Iran kuwa na silaha za nyuklia nchi hiyo inapaswa izingatiwe kama taifa lenye silaha hizo.

Gazeti la Saarbrücker linakumbusha kwamba sera ya mjeledi na diplomasia ilitumiwa na jumuiya ya kimataifa kumlazimisha Gaddafi aachane na mpango wake wa nyuklia. Kwa nini mkakati huo usitumike sasa dhidi ya Iran. Gazeti hilo linauliza? Gazeti hilo linasema, licha ya kuwapo mashaka juu ya njia ya kutumia vikwazo,njia hiyo inaweza kuthibiti kuwa ya ufanisi. Ikiwa Iran itaunda bomu la nyuklia, hatua hiyo itasababisha mashindano ya kuunda silaha katika Mashariki ya Kati. Jumuiya ya kimataifa itakuwa inafanya kosa, ikiwa itayapuuza anayoyasema Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad.

Sasa badala ya kutumia njia ya kijeshi dhidi ya Iran ,vikwazo thabiti ingekuwa njia nyingine, mradi vinatekelezwa kwa moyo wote.

Lakini mhariri wa gazeti la Augsburger Allgemeine anasema Iran pekee ndiyo inayoweza kuuondoa mvutano.Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kwamba njia ambayo Iran inaweza kuitumia ili kuundoa mvutano huo ni kuwaruhusu wakaguzi wa kimataifa wafanye kazi yao bila ya vipingamizi katika vituo vyote vya kinyuklia. Hiyo ni kanuni ya kawaida duniani kote. Lakini kwa nini Rais Mahmoud Ahmadinejad hataki kuwaruhusu wakuguzi hao, inafahamika. Analo analolificha. Kilichobakia kwa jumuiya ya kimataifa ni kutumai kwamba mambo hayatachelewa kabla ya kuchukua hatua za mabavu ili kuilamizisha Iran iachane na mpango wake wa nyuklia.

Mgogoro wa madeni bado unawatoa jasho viongozi wa nchi za Ulaya.Hali ya wasi wasi bado inaendelea. Na sasa wataalamu wametoa ripoti juu ya hali ya uchumi barani Ulaya. Mhariri wa gazeti la Der nue Tag anaizungumzia ripoti hiyo.

Anasema ripoti hiyo inatisha nchi za Ulaya zimeshatumia fedha nyingi ili kuvuta muda tu. Nchi za Ulaya bado hazijalipata jawabu thabiti la mgogoro wa madeni. Mkataba juu ya kulipa madeni uliopendekezwa na wataalamu hao siyo mwarobaini yaani dawa ya maradhi yote!. Lakini ni njia inayoweza kukubalika, badala ya kutumia ulaghai wa mahesabu.!

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri/Abdul-Rahman