1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya31 Julai 2012

Wahariri wa magazeti leo wanazugumzia juu ya mgogoro wa madeni barani Ulaya,mgogoro wa Syria na mvutano baina ya wanamuziki vijana, na Rais Putin nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/15h18
Wanamuziki wa bendi ya "Pussy Riot" wakifikishwa mahakamani
Wanamuziki wa bendi ya " Pussy Riot" wakifikishwa mahakamaniPicha: AP

Gazeti la "Der neue Tag" linazungumzia juu ya mgogoro wa madeni barani Ulaya .Mhariri wa gazeti hilo anasema Mwenyekiti wa jumuiya ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro Jean-Claude Juncker anaonekana dhahiri kuwa ametamauka, siyo tu kutokana na hali inayozikabili nchi zilizotingwa na madeni lakini pia hasa kutokana na juhudi zinazotoka kila upande kwa lengo la kuziokoa nchi hizo.

Mhariri wa gazeti la " Der neue Tag" anasema wanasiasa wote, pamoja na wa Ujerumani wanaushughulikia mgogoro wa madeni chini ya kauli mbiu inayosema, kila anaeweza ajiokoe mwenyewe.Wanasiasa hao wanayajali maslahi yao na siyo yale ya Umoja wa sarafu ya Euro au ya Umoja wa Ulaya.

Mhariri wa gazeti la "Volksstimme" pia anatoa maoni juu ya mgogoro wa madeni. Na anasema Wakati hali inaonekana kuwa ya matumaini nchini Ireland, Ureno,Uhispania na Cyprus, mambo yanaendelea kuwa mabaya nchini Ugiriki. Upanga unaning'inia.Na unanolewa na baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani kama waziri wa uchumi Philipp Rösler aliesema kuwa sasa hakuna hofu tena , ikiwa Ugiriki itajitoa kwenye Umoja wa sarafu ya Euro.Swali la kuulita sasa, ni wakati gani upanga huo utaanza kufanya kazi.Lakini mustakabal wa Ugiriki utajulikana mwishoni mwa mwezi ujao, baada ya pande tatu zinazowasiliana na nchi hiyo kutoa uamuzi.

Hali inazidi kuwa mbaya nchini Sryia. Mapigano yanasababisha idadi kubwa ya wakimbizi wa nchi hiyo katika nchi za jirani. Mhariri wa gazeti la "Süddeutsche" anasema mwenye dhamira ya kweli anaweza kuvikomesha vita vya nchini Syria.Mhariri huyo anaeleza kuwa wakimbizi wa Syria wanapeleka matatizo katika nchi za jirani.Jordan imeishalemewa na wakimbizi hao,nchini Lebanon kinachosuburiwa ni cheche tu ili moto uwake. Anaetaka kuvikomesha vita vya nchini Syria anapaswa kusaidia leo.Na katika hilo, Urusi haiwezi kujiweka kando.

Gazeti la "Rhein Neckar"linatoa maoni juu ya wanamuziki waliofikishwa mahakamani nchini Urusi kwa kosa la kumpinga Rais Putin.Akina dada watatu wa bendi inayoitwa Pussy Riot"wanaweza kupewa adhabu ya miaka saba jela, kila mmoja wakipatikana na hatia. Mhariri wa gazeti la "Rhein-Neckar" anasema kufikishwa mahakamani kwa wanamuziki hao kunathibitisha ni kwa kiasi gani, Urusi bado ipo mbali na utawala wa kisheria!

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Abdul-Rahman