1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya7 Agosti 2012

Wahariri wanatoa maoni juu ya chombo cha anga cha Marekani,"Curiosity" kilichotua kwenye sayari ya Mars. Pia wanatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria na mgogoro wa madeni.

https://p.dw.com/p/15lAV
Sayari ya Mars
Sayari ya MarsPicha: picture-alliance/dpa

 Mhariri wa gazeti la "Stuttgarter  Nachrichten" anazungumzia juu ya safari ya chombo cha anga cha Marekani,Curiosity kilichotua salama kwenye sayari ya Mars 

Mhariri wa gazeti hilo anasema, safari  ya chombo hicho inaonyesha kuwa Marekani inahitaji kuwa na matumaini ya siku za usoni na pia inahitaji kuwa na malengo yanayoonyesha hali ya kipekee ya nchi hiyo. Lakini muhimu zaidi, nchi hiyo inahitaji kuonyesha ushindi. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linasema kwa ufupi, kuwa safari ya chombo cha anga cha Marekani Curiosity,ni ishara ya matumaini kwa Marekani. Umuhimu wake ni mkubwa zaidi kuliko mafanikio ya kisayansi.

Mhariri wa gazeti la "Badische" anakubaliana na hoja hiyo kwamba safari ya chombo cha "Curiosity kwenye sayari ya Mars ni ishara ya matumaini. Lakini mhariri wa gazeti la " Landeszeitung" pia anayatilia maanani  mafanikio ya kutua kwenye sayari ya Mars. Lakini katika maoni yake anakumbusha jambo muhimu kwamba binadamu anajua mengi zaidi juu ya mfumo wa sayari kuliko juu ya mambo ya karibu ,kama vile maziwa  na mfumo wa ikolojia. Masuluhisho mengi yanaweza kupatikana hapa  duniani kuliko kwenye sayari ya Mars.

Gazeti la "Berliner Morgenpost" linatoa maoni juu ya kauli ya Waziri Mkuu wa Italia Mario Monti. Monti ameshauri kwamba katika kuushughulikia mgogoro wa madeni, serikali za Ulaya ziyaweke kando mabunge ya nchi zao. Juu ya kauli hiyo gazeti  la "Berliner Morgenpost" linasema anaefikiria kwamba anaweza kuutatua mgogoro wa madeni kutokea kwenye ngazi za juu,anakosea sana.Anaewapuuza wabunge, hatimaye anawapuuza wapiga kura yaani wananchi.

Mhariri wa"Westdeutsche Zeitung" anazungumzia juu ya mgogoro wa Syria kwa kutilia maanani kwamba utawala  wa Bashar al-Assad unakaribia mwisho.Hata hivyo anasema matokeo ya vita vya nchini Syria hayatakuwa wazi na anaeleeza  kwamba zimebakia wiki,kama siyo siku, kabla ya utawala wa Assad kusambaratika. Lakini swali la kuliuliza sasa, ni jee, ni bendera ya rangi gani itakayopepea baada ya  Assad kuondoka?

Gazeti hilo linasema sasa suala siyo tena kuumg'oa Dikteta.Vita vya nchini Syria siku nyingi vimegeuka kuwa vya kidini na vya kiwakala.Wananchi hawana habari juu  ya shabaha ya vita hivyo.Mambo yanatokea nyuma yao.Matokeo yake yatakuwa ya hatari kubwa kwa eneo lote la mashariki ya kati.

Mwandishi:Mtullya abdu /Deutsche Zeitungen/

Mhariri: