1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya20 Agosti 2014

Wahariri wanaiangalia ziara ambayo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajia kuifanya nchini Ukraine. Pia wanazungumzia juu ya maradhi ya Ebola na sakata la Ferguson.

https://p.dw.com/p/1Cxzl
Baada ya Latvia Kansela wa Ujerumani anatarajia kuizuru Ukraine
Baada ya Latvia Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajia kuizuru UkrainePicha: Reuters

Mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau" anasema Kansela Merkel anaenda Ukraine wakati ambapo majeshi ya nchi hiyo yanapambana na waasi wa mashariki wanaoungwa mkono na Urusi. Mhariri huyo anasema anatumai mgogoro huo siku moja utamalizika na Ukraine na Urusi zitatazama tena ana kwa ana. Hata hivyo katika ziara yake nchini Ukraine Bibi Merkel atapaswa auwasilishe ujumbe wa maridhiano kwa pande zinazopingana sasa.

Putin na Poroshenko

Naye mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anatilia maanani kwamba ziara ya Kansela Merkel itafanyika wakati ambapo Rais Putin wa Urusi na Poroshenko wa Ukraine wanatarajiwa kufanya mazungumzo katika mji mkuu wa Belarus,Minsk, japo bado haijajulikana iwapo watayafanya mazungumzo hayo ana kwa ana.Lakini mhariri huyo anasema hatua hizo zinaleta matumaini juu ya kuutatua mgogoro wa Ukraine.

Naye mhariri wa "Süddeutsche" anaendeleza hoja juu ya mkutano baina ya Putin na Poroshenko.Anasema ni wazi kwamba, baadhi ya watu nchini Ukraine watazikunja nyuso zao juu ya mkutano huo . Wanauliza jee Rais wao kweli anataka kukutana na mtu anaewasaidia waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine? Jee watu 2000 wamekufa bure?Licha ya mashaka hayo, ni ishara nzuri kwamba marais wa Urusi na Ukraine wanakutana.

Maradhi ya Ebola

Maradhi ya Ebola yamezikumba nchi kadhaa barani Afrika na hasa magharibi mwa bara hilo. Gazeti la "Neue Presse" linasema laiti Shirika la Afya Duniani,WHO lingechukua haraka, hatua zinazostahili,ingeliwezekana kuzuia kuenea kwa maradhi hayo.

Gazeti la "Donaukurier" linatoa maoni juu ya sakata la Ferguson nchini Marekani ambako kijana mmoja mweusi alipigwa risasi na polisi mweupe na kuuawa.Mhariri wa gazeti hilo anaungalia mkasa huo katika muktadha wa muhula wa Rais Barack Obama na anasema aliposhinda uchaguzi mnamo mwaka 2008 Obama alikuwa na dhamira ya kuibadilisha Marekani.Lakini leo dunia nzima inashuhudia jinsi alivyonyongea,siyo tu juu ya mkasa wa kijana alieuawa na polisi,Michael Brown. Bila shaka Obama atafurahi ,muhula wake wa pili utakapomalizika ,miaka miwili ijayo.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deustche Zeitungen

Mhariri:Yusuf Saumu