1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wakubaliana

Admin.WagnerD23 Septemba 2015

Wahariri wanatoa maoni juu ya uamuzi wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya wa kugawana wakimbizi. Pia wanazungumzia juu ya kashfa ya kampuni ya magari ya Ujerumani, Volkswagen

https://p.dw.com/p/1GazT
Meneja Mkuu wa Volkswagen Martin Winterkorn
Meneja Mkuu wa Volkswagen Martin WinterkornPicha: Kürsat Akyol

Juu ya uamuzi wa kugawana wakimbizi miongoni mwa nchi za Ulaya uliofikiwa jana na mawaziri wa mambo ya ndani,Mhariri wa gazeti la "Badische" anasema kawia lakini ufike. Mhariri huyo anasema uamuzi huo umechelewa lakini umefikiwa.

Hata hivyo, mhariri wa gazeti la "Eisenacher Presse" anatilia maanani kwamba uamuzi wa kugawana wakimbizi120,000 miongoni mwa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya ulifikiwa kwa makeke. Na kwa hivyo hautatoa mchango katika ustawi wa Umoja wa Ulaya.

Mhariri huyo anafafanua kwa kusema ikiwa malalamiko ya wanachama fulani yatakuwa makubwa, siku moja wanachama hao wataanza kuwa na mashaka juu uanachama wao katika Umoja wa Ulaya.

Mhariri wa gazeti hilo anasema ni muhimu kutambua kwamba baadhi ya nchi hazikujiunga na Umoja huo kwa sababu ya kuvutiwa na maadili ya jumuiya hiyo bali ni kutokana na sababu za kiuchumi. Lakini swali ni nini kitatokea ikiwa mavuno hayo ya kiuchumi yatakauka?

Meneja Mkuu wa kampuni ya Volkswagen atakiwa aondoke

Sakata la kampuni ya magari ya Ujerumani, Volkswagen,bado linaendelea. Kampuni hiyo imekiweka katika magari yake ,kifaa kilichokuwa kinatoa vipimo vya uwongo juu ya kuchafuka kwa mazingira. Meneja mkuu wa kampuni hiyo, Martin Winterkorn, ameomba radhi.

Deutschland IAA Frankfurt Martin Winterkorn
Picha: picture-alliance/dpa/F.v. Erichsen

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema ni jambo linaloeleweka kwamba Meneja Mkuu huyo ameomba radhi. Pia kila mtu alitarajia kwamba atachukua hatua ili kuyaweka bayana yote yaliyotukia.

Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba, ikiwa Meneja Mkuu huyo, bwana Martin Winterkorn anatumai kuendelea kuiongoza kampuni ya Volkswagen licha ya kashfa hiyo kubwa, basi bado hajautambua vizuri uzito wa kashfa iliyotokea.

Naye mhariri wa "Augsburg Allgemeine" anasema ni jambo lisiloeleweka hata kidogo, kwa viongozi wa kampuni ya Volkswagen kuamini kuwa udanganyifu wao usingeliweza kugundulika. Meneja wa kampuni hiyo lazima aondoke ili kuruhusu mwanzo mpya.

Gazeti la "Stuttgarter" linatoa maoni juu ya hali ya nchini Syria,kwa kusema kwamba baada ya miaka mitano tangu kuanza kwa vita nchini Syria,nchi za magharibi sasa zinapaswa kuchagua baina ya magaidi na utawala wa Assad. Ikiwa itawezekena kumzuia Assad kuwashambulia watu wake kwa mabomu,kwa njia ya mazungumzo, mawimbi ya wakimbizi kutoka Syria yatapungua mara moja.

Pamoja na hayo gazeti hilo linaeleza Rais wa Urusi Vladimir Putin anaweza kuhoji kwamba uwepo wa majeshi yake utazuia ushawishi wa Hizbollah na Iran. Na ikiwa amani itapatikana nchini Syria basi, itakuwa baada ya Urusi na Iran kutia saini.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef