1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha mrengo mkali, NDP kupigwa marufuku?

Admin.WagnerD4 Machi 2016

Magazeti ya Ujerumani leo yanatoa maoni juu ya hukumu inayotarajiwa kutolewa na mahakama ya katiba ya Ujerumani kuhusu kukipiga marufuku chama cha NDP cha mafashisti mamboleo

https://p.dw.com/p/1I4kQ
Mahakama Kuu ya katiba ya Ujerumani mjini Karlsruhe
Mahakama Kuu ya katiba ya Ujerumani mjini KarlsruhePicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Wahariri wa magazeti pia wanatoa maoni juu ya wakimbizi wa Afrika Kaskazini wanaorudishwa kwao baada ya kushindwa kupata hifadhi nchini Ujerumani.

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema chama cha mafashisti mamboleo cha National Democratic kimo katika vyombo vya habari kwa mara nyingine .Mahakama kuu ya Ujerumani leo , kwa mara nyingine inasikiliza maombi juu ya kukipiga marufuku chama hicho.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba wanachama wa chama hicho wanao uwezo kujijenga upya kwa namna mbalimbali. Mhariri huyo anatilia maanani aliyosema Waziri wa sheria Heiko Maas kwamba itikadi ya kifashisti haitatoweka kwa kukipiga marufuku chama hicho cha NDP.

Mhariri wa "Thüringische Landeszeitung" anatahadharisha kwamba, litakuwa kosa kuamini kwamba itikadi ya mrengo mkali wa kulia itaondoka katika vichwa vya watu baada ya chama hicho kupigwa marufuku.

Naye mhariri wa "Märkische Oderzeitung" anatilia maanani kwamba hii ni mara ya pili, maombi ya kuwapiga marufuku mafashisti mamboleo hao yanatolewa.


Hata hivyo mhariri huyo anasema kwa kuyawasilisha maombi hayo, mawaziri wa mambo ya ndani wa majimbo yote ya Ujerumani wanakiri kwamba wanayo matatizo .Swali ni, jee mambo mangapi yatapigwa marufuku ili itikadi kali iweze kuondoka?

Wakimbizi wanapaswa kusaidiwa na siyo kushambuliwa

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia juu ya mikasa ya wakimbizi wanaotoka Afrika Kaskazini walionyimwa hifadhi nchini Ujerumani. Mhariri wa gazeti hilo anasema haitakuwa sawa kwa Ulaya kuwatelekeza watu hao.

Wakimbizi nchini Ugiriki
Wakimbizi nchini UgirikiPicha: DW/R. Shirmohammadi

Mhariri huyo anaeleza kwamba kwamba sera ya wakimbizi barani Ulaya isiwe na maana ya kujenga kuta ndefu zaidi ili kujihami dhidi ya wakimbizi. Sera hiyo inaweza kuwa na madhara. Mfano ni kile kinachotokea nchini Libya ameeleza mhariri huyo.

Ikiwa pana haja ya kuwaruhusu wahamiaji kuingia katika soko la ajira barani Ulaya, utaratibu huo unapaswa kufanyika kwa njia za busara Mchakato wa kuwaruhusu watu hao hauna budi ufanyike kwa makini.


Mhariri wa gazeti la "Trierische Volksfruend" anatoa mwito kwa wadau wote barani Ulaya waonyeshe moyo wa huruma kwa wakimbizi. Anasema wakimbizi siyo wahalifu.Anaeleleza kuwa yeyote mwenye moyo wa kibinadamu hatakubali kuona kile kinachotokea kwa wakimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema hao ni wakimbizi, ni watu wanaostahili kusaidiwa.

Kutumia gesi ya kutoa machozi kunaongeza mateso yanayowasibu wakimbizi .Bila ya gesi hiyo tayari watu hao wanatoa machozi.Umoja wa Ulaya bado una nafasi kwa watu hao.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.