1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Maja Dreyer21 Agosti 2007

Uchaguzi wa rais uliofanyika jana nchini Uturuki, ziara ya waziri wa nchi za nje wa Ufaransa nchini Iraq na ugomvi kati ya wakaazi wa asili ya kihindi na wenyeji wa kijiji cha Muegeln nchini Ujerumani – hizo ndizo mada zinazozingatiwa na wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/CHS5

Kwanza ni maoni ya mhariri wa “Westfälischer Anzeiger” juu ya uchaguzi wa rais huko Uturuki ambako waziri wa nje Abdullah Gül, licha ya kushindwa katika duru hili la kwanza, bado anatarajiwa kushinda:

“Abdullah Gül alisema kitu atakachokipa kipaumbele ni kuleta mwafaka baina ya vyama vyote iwapo bunge litamchagua kuwa rais. Lakini tayari kugombea cheo hiki ni kuwadanganya wabunge, kwani mara iliyopita Gül alipogombea kiti cha urais, Uturuki imeingia katika mzozo mkubwa wa kisiasa. Baada ya uchaguzi mpya, chama tawala cha AKP kimepata nguvu zaidi. Kuitumia nguvu yake kwa mara nyingine tena na kuanzisha mvutano na jeshi linalompinga Abdullah Gül ni ishara kwamba chama hiki kinalenga kupigana kuliko kuridhiana.”

Suala la pili ni ziara ya waziri wa mambo kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner wa Ufaransa nchini Iraq. Mhariri wa “Kölner Stadtanzeiger” anatathmini ziara hiyo ina umuhimu gani. Ameandika:

“Ilikuwa ishara ya urafiki na si zaidi ya hayo. Wadadisi wengi wa mambo ya kisiasa waliitathmini hivyo ziara ya waziri Kouchner nchini Iraq. Lakini ni zaidi ya hayo. Kwa kusafiri kwenda Bagdad, waziri Kouchner aliwaonyesha Wairaki kuwa nchi za Ulaya zinajali juu ya hali yao. Hata hivyo, imemchukua Mfaransa miaka minne kufanya safari hii – hiyo basi ni ishara kwamba serikali nyingi za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimeiweka kando Iraq. Ni nchi zile zile ambazo ziliunga mkono vita dhidi ya Saddam Hussein kwa sababu ya hali ngumu iliyowakabili wananchi, lakini tangu kuangushwa Saddam hazikujitolea tena kuwasaidia Wairaqi kuwa na maisha bora.”

Na hatimaye tunaelekea humu nchini na kusoma baadhi ya maoni ya wahariri kuhusu mashambulio dhidi ya Wahindi 50 kijijini Muegeln. Huo hapa ni uchambuzi wa “Mitteldeutsche Zeitung” la mjini Halle:

“Bado chanzo na jinsi mambo yalivyokwenda hakikuchunguzwa, lakini bado ni wazi kwamba ugomvi huo ulisababishwa na chuki dhidi ya wageni – hata ikiwa washambuliaji walilewa sana. Badala ya kuchunguza vizuri tukio hilo, wote wanatoa jibu haraka. Polisi inasema hakuna chuki dhidi ya wageni, na meya wa kijiji hicho anasikitishwa na anasema hakuna kundi la Manazi huko Muegeln.”

Mhariri wa “Rhein-Neckar-Zeitung” analiangalia tukio hilo kutoka pembe nyingine.

“Kila mara tunapopunguza msaada kwa mikoa ya Mashariki tunazungumzia vile eneo la Ujerumani Mashariki lilivyoendelea vizuri: Barabara zimejengwa upya, nyumba zimerekebishwa na nyingine mpya zimejengwa katika miji mikubwa. Lakini nyuma ya utajiri huo na mbali na miji mikubwa kumekuwa hisia za kushindwa katika jamii. Watu wanatumia nguvu kuonyesha hasira zao. Wahanga mara nyingi ni watu wa asili ya kigeni. Lakini hasira siyo dhidi ya wageni bali ni dhidi ya sehemu ya Magharibi ambayo imeiacha nyuma Ujerumani Mashariki bila ya kufahamu matatizo yake.”