1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Maja Dreyer9 Julai 2007

Kwanza katika udondozi wa hii leo ni baadhi ya maoni juu ya mpango wa waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, wa kuongeza juhudi za serikali kujikinga dhidi ya mashambulio ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/CHST

Lakini pendekezo lake la kuiruhusu polisi kuwaua watu wanaotuhumiwa kuwa magaidi limezusha ukosoaji mkali, si tu kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa, bali kutoka kwa wahariri. Kwanza tunasikiliza maoni ya mhariri wa gazeti la “Neue Westfälische”:

“Waziri huyu hakuficha msimamo wake mkali tangu zamani. Lakini yale anayoyadai sana yanaonyesha wazi kuwa lazima mtu huyu asimamishwe. Kuwaua magaidi ni kama kutekeleza tena adhabu ya kifo kupitia mlango wa nyuma.”

Gazeti la “Süddeutsche Zeitung” linamlaani waziri Schäuble kwa kuwadanganya wananchi. Limeandika:

“Waziri huyu anazungumzia kutulia, lakini hatua anazozichukua ni kinyume chake. Anatoa mwito kutokuwa na wasiwasi mno, lakini mwenyewe anaongeza wasiwasi. Analipinga jela la Marekani huko Guantanamo kwa kuwa ni dhidi ya sheria, lakini mwenyewe anapendekeza hatua zinazokumbusha hali kama ya Guantanamo. Hayo yote hayaendi sambamba na sheria ya uhuru wa wananchi.”

Ni gazeti la “Süddeutsche Zeitung”.

Suala la pili: Burudani za “Live earth” zilizofanyika mwisho wa wiki iliyopita zimesikilizwa na kushuhudiwa na watu wengi duniani kote, wakiwa wanatembelea mahala pa muziki kwenyewe au kuziangialia konseti kupitia televisheni. Wahariri leo wanachambua ikiwa burudani hizo zilikuwa ni matamasha makubwa tu ya muziki au kweli ziliweza kuwahamasisha vijana kujitolea katika kulinda mazingira. Hili hapa gazeti la “Mannheimer Morgen”:

“Wale waliopinga matamasha hayo ya “Live Earth” walisema: suala la ulinzi wa mazingira tayari linafahamika na kila mtu duniani. Lakini hiyo si kweli. Bado kuna maeneo mengi ulimwenguni ambapo watu hawayafikirii sana mazingira yao. Huenda miito kama ile iliyoandikwa kwenye skrini majukwaani itasaidia kuwafahamusha, hata ikiwa ni mifupi.”

Mhariri wa “Westfälische Nachrichten” katika uchambuzi wake ana mashaka kuhusu wanamuziki wanaojitolea kushiriki bila ya malipo:

“Tunajua kwamba wale walioshiriki kwenye matamasha hayo ni wale wanamuziki maarufu ambao walipanda ndege kubwa ya Concorde kuhudhuria tamasha la “Live Aid”. Katika biashara ya muziki, matamasha haya makubwa ni fursa nzuri kuongeza umaarufu wa wasanii. Kwa hivyo, wanamuziki wanakubali kutolipwa na pia wanakubali kuzima taa nyumbani mara kwa mara ili kulinda mazingira. Hata hivyo lakini: Mamillioni ya mashabiki wamefahamu kuwa suala la ulinzi wa mazingira si tena lengo la wanaharakati wa mazingira tu, bali ni haja muhimu kwa kila mtu.”

Na hatimaye kuhusu matokeo ya “Live Earth” ni gazeti la “Abendzeitung” kutoka mjini Munich:

“La muhimu ni kwamba suala gumu kama mabadiliko ya hali ya hewa linaweza tu kuwagusu watu ikiwa ujumbe unaotolewa kwao ni wazi na rahisi kuufahamu. Muziki unaweza kuwa ni chombo cha habari hizo.”