1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri watoa maoni juu ya uchunguzi wa tuhuma za uhalifu wa kukwepa kodi

Mtullya, Abdu Said27 Februari 2008

Magazeti ya Ujerumani, katika maoni yao yasifu kazi iliyofanywa na idara za sheria katika kufuatilia tuhuma za uhalifu wa kukwepa kodi.

https://p.dw.com/p/DE5e



Idara  za sheria za Ujerumani zinafuatilia kwa uthabiti  wote tuhuma za uhalifu wa kukwepa kodi zinazomkabili aliekuwa meneja wa posta  Klaus Zumwinkel na watu  wengine nchini Ujerumani.  Juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda.



Gazeti  la KÖLNER STADT-ANZEIGER

linazipongeza  idara za sheria kwa kufanya  kazi nzuri hadi sasa.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ushahidi uliopo ni shadidi  kama chuma dhidi ya wahalifu . Anatilia maanani kuwa licha ya kiasi cha fedha  kilichohusika katika uhalifu huo kuthibitika  kuwa ni Euro milioni 200,kazi iliyofanywa  na idara za upelelezi imeleta  matunda.Hapo awali kiasi kilichotuhumiwa kilikuwa Euro Bilioni nne.

Gazeti linasema utaratibu wa kuweka data  kwenye kitengo cha shirika la upelelezi umethibiti kuwa wa mafakinio.

Na mhariri wa gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU anazipongeza  idara  za sheria Ujerumani kwa kueleza kuwa ingawa hatua  iliyofikiwa hadi sasa haionekani kuwa ya kusisimua kulinganisha na ukubwa wa tuhuma za hapo mwanzoni ,idara za sheria za Ujerumani  zimeonesha jinsi zinavyofuatilia kwa moyo wote uhalifu wa kukwepa kodi.Katika maoni yake mhariri pia anatilia  maanani kuwa maafisa wa idara hizo walianza kwa kufanya msako kwenye nyumba ya mtuhumiwa mkuu, Klaus Zumwinkel aliekuwa  meneja wa Posta.

Mhariri anasema juhudi za maafisa hao zimewatikisa mabwana na mabibi fulani hadi Liechtenstein.

Lakini gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE , pamoja na kusifu hatua iliyofikiwa hadi sasa katika uchunguzi, linasikitika  kwamba watu waaminifu siku zote ndio wanaopunjika.

Gazeti linasema anaelipa kodi wakati unaotakiwa  na kwa kufuata taratibu zilizopo hana anachoambulia kutoka kwa wanakwepa kodi ,badala yake akiba yake ya benki itamulikwa na  biashara  zake vilevile zitapigwa darubini zaidi na zaidi.


Kwa  upande  wake  Gazeti la STUTTGARTER -ZEITUNG linasema hatua zilizochukuliwa na idara za sheria za  Ujerumani katika  kufuatilia tuhuma za  uhalifu wa kukwepa kodi zitachangia katika  kuwafanya wananchi wawe waaminifu na katika maoni yake gazeti la SWARZWÄLDER BOTE linalosema shimo ambamo wahalifu wamekuwa wanaficha fedha sasa limetifuka-shimo hilo ni Liechtenstein.