1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wazungumzia juu ya maafa nchini China.

Mtullya, Abdu Said14 Mei 2008

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya maafa ya nchini China.

https://p.dw.com/p/Dzlg
Magazeti na picha za maafa ya tetemeko la ardhi nchini China.Picha: picture-alliance/ dpa

China imekumbwa na tetemeko la ardhi kubwa na maalfu ya watu wanaendelea kufa.Maafa hayo yanazingitwa pia na wahariri katika maoni yao leo.

Wahariri hao leo pia wanazungumzia juu ya maafa yaliyoikumba Mynamar, na juu ya maadhimisho ya miaka 60 tokea kuundwa kwa nchi ya Israel.

Juu ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi nchini Chinagazeti la Flensburger linasema katika maoni yake kuwa msaada kutoka nje sasa unahitajika nchini China,vinginevyo kitakuwa kifo cha kujitakia.

Mhariri wa gazeti hilo anatanabahisha kwamba utawala wa Beijing unakusudia kutumia maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi kwa malengo ya kisiasa.Utawala huo unataka kuionesha jumuiya ya kimataifa jinsi unavyojali haki,utandawazi na ubinadamu.Misaada kutoka nje inawapa misuli watawala wa China.

Lakini gazeti linasisitiza katika maoni yake kuwa jambo muhimu ni kuwashughulikia watu waliofikwa na maafa badala ya siasa. Mhariri anasema shida inaleta mshikamano na mshikamano unajenga urafiki.

Gazeti la Thüringer Allgemeine pia linazungumzia juu ya China, kwa kuzingatia suala la Tibet.Mhariri wa gazeti hilo anasema, pamoja na kukabiliwa na wakati mgumu kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi, China inapaswa kukumbushwa na jumuiya ya kimataifa juu ya suala la haki za binadamu katika jimbo lake la Tibet.

Gazeti la Der Neue Tag linatoa maoni juu ya msimamo wa watawala wa Mynamar kuhusu misaada ya kimataifa, kwa ajili ya kukabiliana na maafa yaliyosababishwa na kimbunga Nargis.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa majenerali wanaoitwala Mynamar ni watu wasiojiamini, kwa sababu hawafanyi linalohitajika katika wakati mujarab. Wanachoweka mbele ni utawala wao badala ya kuwashughulikia wananchi wao waliofikwa na maafa ya kimbunga.

Gazeti la Berliner Morgenpost linatoa maoni juu ya maadhimisho ya miaka 60 ya nchi ya Israel.Gazeti hilo linasema kuundwa nchi ya Israel miaka mitatu tu baada ya maangamizi ya wayahudi barani Ulaya,kulitimiza ndoto ya wayahudi.Pamoja na makosa yote yaliyofanywa na Israel,katika miaka sitini,kuwapo kwa nchi hiyo hadi leo ni muujiza.