1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said22 Julai 2008

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya seneta Obama wa Marekani.

https://p.dw.com/p/EhVK
Mgombea kiti cha urais nchini Marekani seneta Barack Obama anaetarajiwa kuwasili Ujerumani alhamisi ijayo.Picha: AP

Wahariri  wa  magazeti ya  Ujerumani leo wameandika  kwa  mapana na marefu juu ya seneta wa Illinois Barack Obama  anaegombea kiti cha urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha demokratik. Obama anatarajiwa  kuanza ziara alhamisi ijayo nchini Ujerumani.


Lakini  wahariri  wengine hawajasahau suala linalowahusu zaidi wajerumani wote-   yaani uchumi wa nchi. Baadhi wanasema  uchumi wa  Ujerumani unaonesha  dalili za kuanza kurudi nyuma.

Juu ya seneta  Barack Obama, 

gazeti  la Der neue  Tag linasema theluthi mbili ya Wajerumani wangelimpigia kura  Obama. Ni asilimia 10 tu ya wajerumani wangelimpa kura zao mshindani wake John McCain. Lakini mhariri wa  gazeti  hilo anatilia maanani kwamba  uchaguzi  unafanyika Marekani na siyo nchini Ujerumani. Ndiyo kusema haiwezekani kumpuuza John McCain.

Lakini mhariri wa  gazeti la  Kölnische Rundschau  anasema  angalau, Obama anatambua  changamoto za nyakati  za sasa.

Gazeti hilo linaeleza kuwa uwanja wa mapambano dhidi ya magaidi wa Alkaida upo  katika maeneo ya Hindukush  kwenye mpaka na  Pakistan. Obama ametambua hayo.

Lakini  gazeti linasema ,ni vigumu kuwasilisha ukweli huo kwa  utawala wa  Bush.

Gazeti la Bild Zeitung  linazungumzia juu ya uchumi  wa Ujerumani, na linasema  kuwa  ishara  zilizopo juu ya uchumi  huo siyo nzuri.

Gazeti linasema masoko ya hisa yanaserereka, bei ya mafuta inaongezeka  na sasa  zinafuatia vurumai  za uchumi wa dunia zinazoathiri uchumi wa  Ujerumani. Mhariri  anasema  pamoja  na hayo yote uchumi wa  Ujerumani  bado  unaonesha maajabu. Lakini, kuanzia mwaka kesho hali  itakuwa nyingine. Ishara zinaonesha kuwa ustawi  utanywea. Mawingu  yanaaashiria kuwa patakuwa na dhoruba  mwakani, katika uchumi wa Ujerumani.

Gazeti la Badische Zeitung nalo linasisitiza kuwa,athari za kurudi nyuma ustawi wa  uchumi  wa Ujerumani zitaonekana katika soko la ajira.

Mhariri  wa gazeti  hilo anasema huenda  idadi ya wasiokuwa na ajira ikaongezeka  nchini  Ujerumani.Ishara juu ya  uwezekano huo  zinaongezeka.