1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said8 Septemba 2008

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia juu ya mabadiliko ya uongozi katika chama cha SPD.

https://p.dw.com/p/FDVP
Mwenyekiti mpya wa chama cha SPD, Franz Müntefering.Picha: AP

Chama cha Social Demokratik kilichomo kwenye serikali ya mseto hapa nchini Ujerumani kimefanya mabadiliko katika uongozi wake wakati umebakia mwaka mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.


Chama hicho kimemchagua Frank Walter Steinmeier kukiwakilisha , katika uchaguzi mkuu mwakani. Steinmeier ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje ni makamu mwenyekiti wa chama hicho. Chama cha SPD pia kimemrudisha Franz Müntefering kuwa mwenyekiti wake.


Juu ya hayo gazeti la Berliner Morgenpost linasema, kuchaguliwa Steinmeier na Müntefering ni hatua ya uwerevu.

Gazeti linasema wanasiasa hao, wana umaaruf mkubwa ndani ya chama cha SPD.


Mhariri wa Fuldaer Zeitung anahoji kuwa uongozi mpya wa chama cha SPD maana yake ni kukiweka mbali chama hicho na wakomunisti wa zamani.

Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza katika maoni yake kwamba kuchaguliwa ,Steinmeier na Müntefering kukiongoza chama cha SPD ndiyo njia peke ya kukipa chama hicho wajihi wa pekee.


Lakini mhariri wa gazeti la Reutlinger General Anzeiger anasema mabadiliko yaliyofanyika jana hayatokani na sababu za kimkakati bali hiyo ilikuwa operesheni ya dharura ya kuokoa maisha ya mgonjwa.

Mhariri wa Reutlinger General Anzeiger anasema mgonjwa huyo siyo chama cha SPD tu. Anaeleza kuwa mgogoro unaokikabili chama cha SPD unaweza kudodoswa kuwa ni ishara ya mgogoro wa mfumo wa kisiasa unaoikabili nchi nzima ya Ujerumani.

Hatahivyo mhariri wa gazeti la Braunschweiger anasema kuchaguliwa Steinmeier , kupambana na Angela Merkel wa CDU, katika kugombea ukansela wa Ujerumani mwakani, ni hatua sahihi.Na mwenyekiti mpya, Müntefering atasaidia katika maandalio ya kampeni za uchaguzi.