Wahariri wazungumzia juu ya elimu.
10 Septemba 2008
Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya ripoti kuhusu kiwango cha elimu nchini Ujerumani iliyotolewa na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendelo OECD.
Gazeti la Aachener Nachrichten linasema mfumo wa elimu wa Ujerumani unakabiliwa na matatizo kwa sababu ya muundo wa shirikisho.Ujerumani ina majimbo 16 na kila jimbo lina utaratibu wake wa elimu.
Hatahivyo gazeti linasema dawa ni moja tu- kuongeza bajeti ya sekta hiyo.
Na mhariri wa gazeti la Honnoversche Allgemeine analalamika kwamba kinachofanyika sasa hakitoshi katika kurekebisha hali ya elimu nchini Ujerumani.
Mhariri huyo anasema jambo baya zaidi kwa Ujerumani ni, kwamba wasomi wanatoeka nchini.
Gazeti linasema habari hizo ni za kushtusha kwa wote wanaoitakia mema Ujerumani, kwani nchi isiyokuwa na watu wenye ujuzi asilani haitaweza kushindana na nchi zingine duniani.
Gazeti la Südwest Presse pia
limetathmini ripoti ya shirika la
ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo
OECD, juu ya kiwango cha elimu
nchini Ujerumani.
Gazeti hilo linasema , ripoti hiyo inaonesha kuwa kwa mara nyingine Ujerumani imeanguka katika mtihani wa elimu. Gazeti limekariri ripoti iliyotolewa hivi karibuni inayoonesha kuwa Ujerumani ipo nyuma katika kutoa fursa za kujiendeleza kwa watu wenye elimu ya chini kulinganisha na nchi zingine za Umoja wa Ulaya.
Mhariri wa gazeti Südwest Presse anasema suluhisho ni kuongeza fedha kwa ajili ya elimu.