1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya12 Machi 2009

Wahariri wa magazeti wataka sheria kali kudhibiti umilikaji wa silaha nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/HAVc
Kijana alieua watu katika jimbo la Baden Würtemberg jana.Picha: ap

Wahariri wa magazeti karibu yote wanazungumzia  juu ya mkasa  wa kusikitisha uliotokea jana katika jimbo la kusini magharibi mwa Ujerumani,Baden Würtenberg.

Kijana mmoja aliekuwa na umri wa miaka17 aliingia katika shule moja iliyopo katika mji wa Stuttgart, kusini magharibi mwa Ujerumani, na kuanza kufyatua risasi kila upande. Aliua watu 16 wanafunzi na  walimu kabla yeye mwenyewe kupigwa  risasi na polisi.

Sasa watu  wanauliza ilikuaje, kwa nini,nani anabeba dhamana  ya kosa hilo.

Mhariri wa gazeti la Südkurier anasema jambo moja  limeshabainika  wazi  kabisa kwamba kijana huyo  alipata silaha kutoka kwenye kabati la  baba  yake.


Mhariri huyo anakiri katika maoni yake kwamba kila kitu ni halali kabisa  juu ya silaha aliyotumia kijana huyo, kwa sababu Iliorodhoshwa kwa mujibu wa sheria. Lakini anasema,silaha hiyo ilikuwa mahala ambapo iliweza kuingia katika mikono ya mtu asiestahili kuipata.

Ndiyo sababu mhariri huyo anataka sheria za kudhibiti umilikaji wa silaha ziwe kali  zaidi.

Gazeti la Neue Westfällische  pia linasisitiza hayo.

Lakini  mhariri wa gazeti hilo anasema, kabla ya kuanza kupitisha  sheria kali,lazima watu waulize,  kwa nini silaha nyingi zinazunguka katika mikono  ya watu nchini.

Mhariri amekariri takwimu  za polisi zinazoonesha kuwa bunduki na pistola milioni10  zimeorodheshwa  kisheria, lakini nyingine milioni kumi  zimo katika mikono ya watu kinyume cha  sheria.

Pamoja  na hayo mhariri  anatilia maanani kwamba mlikuwa na bunduki 15  nyumbani kwa  wazazi wa kijana muuaji.

Gazeti la Cellesche nalo pia linatoa mwito wa kupitishwa  sheria kali.Lakini gazeti hilo linasema  sheria hizo lazima zitekelezwe kwa moyo wa dhati.

Na mhariri  wa gazeti la Abendzeitung, anasema ili  kuepusha  maafa  kama hayo yaliyotokea  katika mji wa Stuttgart pana haja kwa walimu na polisi kutafakari njia za kuwasaidia vijana wenye  mwelekeo  wa kuwa hatari.